MSHAMBULIAJI wa Yanga, Simon Msuva juzi aling’ara katika hafla ya
kukabidhi tuzo za Ligi Kuu msimu wa mwaka 2014/2015 baada ya kunyakua
tuzo mbili.
Msuva, ambaye kwa sasa yupo Misri na timu ya Taifa, Taifa Stars,
alipata tuzo ya Mfungaji bora baada ya kufunga mabao 17 na tuzo ya
mchezaji bora.
Tuzo ya mchezaji bora ilikuwa pia inawaniwa na Mohamed Hussein (Simba
SC) na Mrisho Ngassa wa Yanga. Kwa kunyakua tuzo hizo, Msuva amepata Sh
milioni 11.4, kila tuzo ikiwa ni Sh milioni 5.7.
Tuzo hizo zilipokewa na wazazi wake kwa niaba yake. Aidha, tuzo ya
kipa bora ilienda kwa golikipa Shaaban Kado aliyedakia Coastal Union
msimu uliopita, kwa sasa amesajiliwa na Mwadui FC.
Amepata Sh milioni 5.7. Wengine waliokuwa wakiwania tuzo hiyo ni Mohamed Yusuph (Prisons) na Said Mohamed (Mtibwa Sugar).
Kocha Mbwana Makata wa Prisons ndiye aliyeondoka na kitita cha Sh
milioni 8.6 baada ya kunyakua tuzo ya kocha bora akiwazidi Goran
Kopunovic (Simba SC) na Hans Van Der Pluijm (Yanga).
Makata amepewa tuzo hiyo kwa kuinusuru Prisons kushuka daraja. Kiasi
kama hicho cha fedha kimeenda pia kwa mwamuzi Israel Nkongo aliyepata
tuzo ya mwamuzi bora na kuwapiku wenzie Jonesia Rukyaa na Samwel Mpenzu.
Mtibwa Sugar nayo ilijinyakulia Sh milioni 17.2 kwa kutwaa tuzo ya timu yenye nidhamu, ikizishinda timu za JKT Ruvu na Simba.
Aidha mabingwa wa ligi hiyo, Yanga walikabidhiwa hundi yao ya Sh
milioni 80.4 kwa kutwaa ubingwa, Azam ilikabidhiwa hundi ya Sh milioni
40.2 kwa kushika nafasi ya pili, Simba Sh milioni 28.7 kwa kuwa wa tatu
na Mbeya City Sh milioni 22.9 kwa kushika nafasi ya nne.
Hafla hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa JB Belmonte (Kilimanjaro)
uliopo jengo la Golden Jubilee Tower (PSPF) iliandaliwa na Bodi ya Ligi
Kuu Tanzania (TPLB) kwa kushirikiana na wadhamini wa kampuni ya simu za
mkononi ya Vodacom.
Akizungumza kabla ya kukabidhi tuzo hizo, Naibu Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia aliwaomba wadhamini Vodacom
kuboresha mkataba wao huku akiwasihi wadhamini wenza Azam kuongeza fedha
ili timu zisilalamikie kupungua kwa mapato.
“Mapato ni lazima yapungue, watu hawaji uwanjani, kwa hiyo naomba
niwaombe Azam najua wanaweza, wamalizie kabisa ile asilimia 40 ili timu
zifidie… kingine kinachochangia kushuka kwa mapato ni upangwaji wa
ratiba ya ligi, huwezi kuipanga Simba icheze leo Yanga icheze kesho,
huwezi kupata mashabiki, maana watazamaji ni walewale, muwe mnapanga
kama Yanga inacheza hapa (Dar es Salaam) leo basi Simba ikacheze hata
Mtwara,” alisema.
No comments:
Post a Comment