TFF haitambui uamuzi wa Simba

https://hivisasa.co.tz/wp-content/uploads/2015/05/Mwesigwa-Malinzi.jpg
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Mwesigwa Selestine
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema halitambui tamko lililotolewa na Klabu ya Simba kwa mchezaji wake Ramadhan Singano hadi watakapopeleka barua ya maandishi.
Simba na Singano zina mgogoro wa kimkataba ambapo mchezaji huyo anadai amemaliza mkataba wake wa miaka miwili, lakini Simba inadai kuwa mchezaji huyo bado halali kwao, kwani alisaini mkataba wa miaka mitatu unaotarajiwa kumalizika Julai mwakani.
Mgogoro huo ndio uliofanya TFF kuwaita meza moja na kubaini kuna tatizo kwenye mikataba yote, hivyo kuwaamuru wajadiliane upya.
Katika taarifa ya Rais wa Simba, Evans Aveva kwa waandishi wa habari juzi, kikao cha Kamati ya Utendaji kiliamua kutokutana na Singano na kwamba inamtambua mchezaji huyo ni mali yake mpaka Julai mosi mwakani kwa mujibu wa mkataba ambao TFF inayo nakala yake.
Aveva alisema, kamati yake ya utendaji imeamua hivyo kwani mchezaji huyo amekiuka makubaliano ya kwenye kikao cha pamoja na kutangaza kwenye vyombo vya habari kwamba yeye yupo huru.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa TFF Selestine Mwesiga alisema hajapata taarifa za Simba kuhusu kutofanya mazungumzo kama walivyoamriwa.
“Mimi ninachojua Simba na mchezaji wake walikubaliana kwa maandishi sasa kama hawajakubaliana sijapata taarifa, kwani watakachokubaliana ni lazima walete kwa maandishi,” alisema.
Simba katika taarifa yake ilisema kuwa klabu hiyo itafanya mazungumzo na mchezaji huyo pindi muda muafaka utakapofika kwa mujibu wa kanuni baada tu ya kumalizika kwa mkataba wake mwakani Julai.
“Ni matarajio yetu mchezaji Singano ataheshimu maamuzi hayo na mkataba ambao pia upo TFF na kwenye mtandao wa TMS,” alisema taarifa ya Aveva.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved