Jina
la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere limeibuka ghafla na kwa nguvu baada
ya makada wanaowania kupitishwa na CCM kuanza kutangaza nia, huku wengi
wao wakionyesha kuaminiwa na muasisi huyo wa Taifa na wengine kuahidi
kufuata miiko aliyoiweka wakati alipoongoza Serikali ya Awamu ya Kwanza.
Makada
hao pia wamezuru kaburi la Baba wa Taifa na wengine kutumia kuaminiwa
kwake na wananchi wakati akiwa na umri mdogo ili kujenga hoja kuwa
uzoefu na umri si suala la kuzingatiwa katika kupata kiongozi wa
Serikali ya Awamu ya Tano.
Mwalimu
Nyerere, aliyeongoza Tanganyika tangu mwaka 1961 na baadaye Tanzania
kuanzia mwaka 1964 hadi 1985 alipong’atuka, anajulikana sana kutokana na
kuanzisha Azimio la Arusha mwaka 1967 lililoweka miiko ya uongozi bora
na kuweka misingi ya siasa za ujamaa, mambo ambayo yalitenguliwa na
Azimio la Zanzibar miaka michache baada ya kuachia urais.
Mbali na
kutangaza miiko hiyo iliyojenga maadili ya uongozi wakati nchi ikielekea
kujenga Taifa la kijamaa, Mwalimu Nyerere alikuwa na nguvu ya ushawishi
na mkali dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi, jambo lililomfanya
aheshimike ndani na nje ya nchi.(P.T)
Wakati
Taifa likisikiliza hoja za wanaotia nia ya kuwania urais ikiwa ni miezi
michache baada ya Bunge la Katiba kuondoa mambo ya maadili kwenye Rasimu
ya Katiba, suala hilo linaonekana kurudi kwa nguvu kwenye sera za
wagombea uongozi ambao wanataja kila mara jina la Nyerere, miaka 16
baada ya kifo chake.
“Wanamtumia
Nyerere kwa sababu wanajua alikuwa muadilifu, alikuwa akisema kitu watu
wanatekeleza. Leo kiongozi anatoa maagizo hakuna anayetekeleza,”
alisema mchungaji wa Kanisa la Pentekoste, Dk Damas Mukasa alipoulizwa
maoni yake kuhusu kuibuka kwa jina hilo la muasisi wa Tanganyika.
Akitangaza
rasmi nia ya kuutaka urais kwenye hafla iliyofanyika uwanja wa ofisi ya
CCM ya Mkoa wa Lindi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe alisema kuwa anatosha kushika wadhifa huo na
kwamba Mwalimu Nyerere atafurahi huko aliko iwapo atachaguliwa kuwa Rais
kwa miaka 10 ijayo.
Pia,
Membe alisema kuwa Machi mwaka huu alikwenda Butiama na kuzuru kaburi la
Mwalimu Nyerere ambako alipiga magoti na kumweleza nia yake ya kuutaka
urais.
“Nilipiga
goti nikamwambia Mwalimu, navitaka viatu vyako, alivivaa Mzee (Ali
Hassan) Mwinyi, Mzee (Benjamin) Mkapa na (Rais, Jakaya) Kikwete. Sasa
nataka kuvivaa mimi na nina hakika vinanitosha,” alisema Membe.
“Ninaamini
vitanitosha. Nikamwambia chondechonde, kama havitanitosha, niambie...
timu yangu ya mikoani ikawahi kuniambia unatosha.”
Mkurugenzi
mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk Hassy Kitine naye
alitumia jina hilo wakati akitangaza nia ya kutaka kurejea Ikulu ambako
alifanya kazi chini ya utawala wa muasisi huyo, akiahidi kutumia miaka
mitano kuirudisha Tanzania ya Mwalimu Nyerere.
Dk Kitine
alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake aliyoitoa mjini Dodoma kutoa
mifano ya utendaji wa Mwalimu Nyerere na kuwaponda wengine waliojitokeza
kuwa hawana sifa za kumfikia.
No comments:
Post a Comment