Ni bajeti ya kumaliza miradi

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgrtW9gugAWxQUN4a5ahNYgRf3Z0xJRjFkYMhq5bTCKT-ufoi8P8cW1gIRJFt9JuRD4irm0eMqSFW2S1HLw7r0hYdckQcaf09BVeeTpy2eMzDxvVAJF7j8BoVWWeChMoon3bM6Hbyo15PE/s1600/AKISOMA.jpg
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum

BAJETI ya Serikali ya mwaka 2015/16 ambayo imewasilishwa serikalini, inalenga katika kukamilisha miradi iliyoanza kutekelezwa na Serikali na kulinda mafanikio yaliyokwishapatikana katika sekta za elimu, afya, maji na maendeleo ya jamii.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema bajeti hiyo inayotegemewa, itakamilisha miradi kadhaa, kama upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere na ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa Kinyerezi II.
Alisema watajenga ujenzi wa maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 wilaya ya Mbozi na tani 10,000 Songea Mjini, ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi, kuimarisha na kuboresha vitendea kazi na huduma katika reli ya kati.
Miradi mingine ni ujenzi wa Bandari Mpya ya Mbegani mkoa wa Pwani, awamu ya tatu ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, kuendelea na utekelezaji wa Mradi wa Upanuaji wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu na Ruvu Chini na kuandikisha wapiga kura na vitambulisho vya Taifa.
Alisema katika kipindi cha 2015/2016, Serikali imekadiria kutumia jumla ya trilioni 22.5 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Kiasi hicho kinajumuisha Sh trilioni 16.6 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh trilioni 5.9 ni matumizi ya maendeleo.
Mgawanyo wa fedha katika sekta Mkuya alisema mgawanyo wa bajeti katika sekta ambao haujumuishi madeni ya kisekta, yanayolipwa kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali (CFS) ni kama ifuatavyo: Nishati na Madini: Imetengewa Sh bilioni 916.7 (sawa na asilimia 5.7) ya bajeti yote bila kujumuisha Mfuko Mkuu wa Serikali.
Alisema kati ya kiasi hicho, Sh bilioni 447.1 zimetengwa kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa umeme vijijini. Miundombinu: Alisema Sh trilioni 2.4 zimetengwa kwa ajili ya sekta ya ujenzi na uchukuzi sawa na asilimia 15.1 ya bajeti yote, bila kujumuisha Mfuko Mkuu wa Serikali.
Alisema kati ya kiasi hicho, Sh bilioni 322.4 zimetengwa kwa ajili ya miundombinu ya usafirishaji; Sh trilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja; Sh bilioni 9.5 kwa ajili ya kujenga na kuboresha bandari.
Kilimo: Sekta ya kilimo imetengewa Sh trilioni 1 sawa na asilimia 6.2 ya bajeti. Fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, ujenzi wa maghala na masoko katika maeneo mbalimbali nchini.
Elimu: Waziri alisema Sh trilioni 3.9 sawa na asilimia 24.0 ya bajeti yote bila kujumuisha Mfuko Mkuu wa Serikali. Alisema fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya sekta hii ili kugharimia ubora wa elimu na kuimarisha miundombinu ya elimu.
Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 348.3 zimetengwa kwa ajili ya kutoa mikopo ya elimu ya juu. Maji: Kwa upande wa sekta ya maji zimetengwa Sh bilioni 573.5 sawa na asilimia 3.6 ya bajeti yote.
Fedha hizo ni kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji mijini na vijijini. Kwa upande wa afya: Kiasi cha Sh trilioni 1.8 sawa na asilimia 11.3 ya bajeti yote bila kujumuisha.
Fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na ununuzi wa madawa, kuzuia magonjwa ya mlipuko, chanjo za watoto, ujenzi wa zahanati na kudhibiti Ukimwi na malaria.


No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved