SERIKALI imetangaza kuongeza tozo ya mafuta ya petroli na dizeli ili
fedha zitakazopatikana, zikatunishe mfuko wa kusambaza nishati vijijini.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salumu alisema tozo ya mafuta ya dizeli,
imepanda kutoka Sh 50 kwa lita hadi Sh 100 kwa lita, ikiwa ni ongezeko
la Sh 50 kwa lita.
Mafuta ya petroli tozo yake imepanda kutoka Sh 50 hadi Sh 100 kwa
lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 50 kwa lita. Mafuta ya taa kutoka Sh 50
kwa lita hadi Sh 150 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 100 kwa lita.
Mkuya alisema hiyo itasaidia kuondoa uwezekano wa kuchakachua.
Alisema hatua ya kuongeza Tozo ya Mafuta ya Petroli, inatarajiwa
kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh bilioni 139.8.
Alisema fedha hizi zote zitaelekezwa katika Mfuko wa REA 81 kwa ajili
ya utekelezaji wa shughuli za usambazaji wa umeme vijijini.
Mkuya alisema anapendekeza Waziri wa Fedha apewe mamlaka ya kusamehe
Tozo ya Mafuta ya Petroli kwenye miradi inayotekelezwa kwa misaada ya
wafadhili na yenye mikataba isiyohusisha utozaji wa tozo hii.
“ Lengo la hatua hii ni kuondoa usumbufu na ucheleweshaji kati ka
utekelezaji wa miradi kutokana na kutokuwepo kwa mamlaka ya kisheria kwa
Waziri wa Fedha kutoa msamaha wa tozo hii,” alisema.
Ushuru wa mafuta na barabara Juu Mkuya pia alisema wameongeza ushuru
wa mafuta kwa viwango mbalimbali na mafuta ya dizeli kutoka Sh 263 kwa
lita hadi Sh 313 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 50 kwa lita.
Mafuta ya petroli kutoka Sh 263 kwa lita hadi Sh 313 kwa lita, ikiwa
ni ongezeko la Sh 50 kwa lita. Alisema hatua hiyo inatarajiwa kuongeza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh bilioni 136.4.
“Napendekeza kuwa, fedha zitakazopatikana kutokana na ongezeko hilo
la Ushuru wa barabara zitumike katika kugharimia usambazaji wa umeme
vijijini kupitia mfuko wa REA,” alisema.
Mashirika ya umma yabanwa Mkuya alisema taasisi zote za umma
zinazojiendesha bila ruzuku ya Serikali, zitawekewa ukomo wa matumizi
yake ambayo hayatazidi asilimia 60.
Alisema lengo ni kuweka utaratibu utakaosaidia kudhibiti matumizi na
kuyawezesha mashirika na taasisi za Serikali, kuchangia ipasavyo kwenye
Mfuko Mkuu wa Serikali.
“Kwa msingi huo, napendekeza kuweka ukomo usiozidi asilimia 60 ya
mapato kutumika katika matumizi ya uendeshaji na asilimia 70 ya bakaa
itakayopatikana itawasilishwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali,” alisema.
Alipendekeza kuwa mashirika na taasisi nyingine, zilizokuwa
zinachangia asilimia 10 ya mapato ghafi, sasa zichangie asilimia 15
katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Kodi michezo ya kubahatisha juu Mkuya alisema watatoza kodi ya
michezo ya kubahatisha katika zawadi za ushindi kwa kiwango cha asilimia
18 ya zawadi inayotolewa kwa mshindi.
Alisema hatua hii inalenga katika kuongeza wigo wa mapato ya
Serikali. Alisema watatoza ada ya Leseni Kuu ya dola za Marekani 30,000
au kiasi cha Shilingi kinacholingana na hicho kwa uendeshaji wa bahati
nasibu ya kutabiri matokeo ya michezo na kutoza ada ya Leseni Kuu ya
dola za Marekani 10,000 au kiasi cha Shilingi, kinacholingana kiasi
hicho kwa uendeshaji wa michezo ya mashine za kamari.
“Lengo la hatua hii ni kuimarisha usimamizi wa michezo hii inayokua
kwa kasi na kuongeza wigo wa mapato ya Serikali,” alisema. Alisema
wataweka utaratibu wa kutoa hati ya kufaa kwa mwombaji, ambaye baada ya
kupekuliwa na kuonekana kufaa kupewa leseni.
Alisema hati hiyo italipiwa ada ya Sh milioni 1. Mkuya alisema
wataweka utaratibu wa usajili wa vifaa vya michezo ya kubahatisha na
kutoza ada mbalimbali ya usajili.
No comments:
Post a Comment