SERIKALI imeendelea kuwapa ahueni wafanyakazi nchini baada ya
kupunguza kiwango cha Kodi ya Mishahara (PAYE) kutoka asilimia 12 katika
mwaka wa fedha uliopita hadi asilimia 11.
Hayo yalidhihirika jana kupitia Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha
2015/16 iliyosomwa bungeni mjini Dodoma jana na Waziri wa Fedha, Saada
Mkuya Salum. Katika bajeti inayomalizika, Serikali ilipunguza pia kodi
hiyo kutoka asilimia 13 hadi 12.
Ingawa Shirikisho la Wafanyakazi (TUCTA) limekuwa likitaka kodi hiyo
ipungue hadi kufikia asilimia 10, Serikali imekuwa ikipunguza kiwango
hicho kutoka asilimia 18 mwaka 2006/7 hadi sasa kufikia asilimia 11
ambayo ni sawa na punguzo la asilimia 35.
Waziri Mkuya alisema Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha maslahi
ya watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kuongeza mshahara wa kima cha
chini kutoka Sh 65,000 mwaka 2005 hadi kufikia Sh 265,000 mwaka 2014/15
ikiwa ni ongezeko la asilimia 307.7.
Kuhusu pensheni kwa wastaafu, Waziri alisema katika mwaka huu wa
fedha 2015/16, serikali itaongeza kima cha chini cha pensheni kwa
wastaafu wa Serikali kwa mwezi kutoka Sh 50,000 hadi Sh 85,000, sawa na
ongezeko la asilimia 70.
“ Serikali inatambua umuhimu wa wastaafu ambao walitoa mchango mkubwa
kwa taifa hili na ndio maana, kwa kuzingatia hilo, serikali imeongeza
pensheni yao,” alisema.
Akizungumzia mafao kwa wazee, Waziri Mkuya alisema Serikali kwa
kutambua mchango wao pia katika kujenga taifa hili, imedhamiria kwa
dhati kuwalipa mafao ya kila mwezi.
Ili kufanisha zama hiyo alisema serikali imeanza zoezi la kuandaa
mfumo na utaratibu wa kuwatambua wazee wote nchini ili kupata idadi
kamili ya wazee na kuhakikisha kwamba mafao yanawafikia walengwa kwa
wakati.
“Kwa kuzingatia hilo, katika mwaka 2015/16, Serikali inatarajia
kuanza maandalizi ya kuwezesha kufanya malipo hayo. “Maandalizi hayo ni
pamoja na kutunga Sheria stahiki, kuwatambua kupitia Serikali za Mitaa
kwa kutumia mfumo shirikishi jamii na kuweka utaratibu wa kuwalipa,”
alisema.
No comments:
Post a Comment