Pinda afungua mashindano ya Umisseta Taifa

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhxrHg62EoXOLgR-yW_fes3UL-rkocmMFgXVa4UhoF1B5n_ATzDKntI9ruGXv5PKi_2wlCp1xnrJPXQRS9wg2AOmDQxsF9Qj05UXNYDEQOgwJxBWJHK2NhYuJphYYe4CqAJNMntIy-SL1te/s640/IMGL8637.JPGWAZIRI Mkuu Mizengo Pinda jana alifungua rasmi Michezo ya Shule za Sekondari Tanzania (Umisseta), yaliyoanza juzi jijini hapa.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mashindano hayo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, aliwataka watambue kwamba michezo siyo mahali pa ugomvi bali michezo inataka nidhamu na uadilifu.
“Mashindano siyo ugomvi bali ni fursa ya kujenga mshikamano, tumieni fursa hii kujenga dhamira ya kweli ya kutaka kufanya vizuri zaidi katika michuano ijayo,” alisisitiza.
Alisema washiriki wa mashindano hayo wamekutanishwa kutoka mikoa mbalimbali, na kwamba watapimwa siyo tu katika michezo, bali katika masuala mengine ikiwemo uadilifu, usafi, kuzingatia maelekezo na nidhamu.
“Baadhi ya wanamichezo wana mahitaji maalumu, hivyo tuoneshe upendo kwao ili wajisikie nao kushiriki katika mashindano haya,” alisisitiza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa michezo hiyo, Waziri wa Nchi (TAMISEMI), Hawa Ghasia alisema mashindano hayo ni ya tano kufanyika kitaifa tangu yalipofufuliwa mwaka 2000.
Akitoa mchanganuo wa mashindano hayo, Waziri Ghasia alisema mashindano hayo yanayofanyikia Butimba, wilayani Nyamagana yataendeshwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itahusisha mashindano ya UMISSETA yaliyoanza Juni 8,2015 na yanatarajiwa kumalizika Juni 20, mwaka huu.
“Awamu ya pili itakuwa ni ya mashindano ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA), ambayo yanatarajia kuanza Juni 22, 2015 na kukamilika Julai 4, 2015".
UMISSETA inajumuisha washiriki 1,755 wakati UMITASHUMTA itashirikisha wanamichezo 1,000.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved