Hakuna kiingilio tuzo za KTMA (Kilimanjaro Tanzania Music Award) 2015

http://shaffihdauda.co.tz/wp-content/uploads/2015/04/KILI.jpgWAANDAAJI wa tuzo za muziki nchini za KTMA (Kilimanjaro Tanzania Music Award) wametangaza kutokuwepo kwa viingilio kwenye kilele cha utoaji wa tuzo hizo zitakazofanyika Juni 16 kwenye ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Meneja wa bia ya Kilimanjaro wanaodhamini tuzo hizo kutoka kampuni ya bia ya TBL, Pamela Kikuli, alisema wameandaa utaratibu wa kutoa mialiko maalumu kwa baadhi ya watanzania watakaopewa fursa ya kuhudhuria katika tukio hilo.
“Tumepanga utaratibu mpya ikiwemo kutokuwepo viingilio siku ya utoaji wa tuzo lakini tutatoa mialiko kwa baadhi ya watu ambao watapata fursa ya kuwemo kwenye sherehe za utoaji wa tuzo hizo,” alisema Kikuli.
Aidha Kikuli alisema kwa kutambua watanzania wengi wanataka kuzishuhudia tuzo hizo, wamepanga tuzo hizo zirushwe moja kwa moja kwenye kituo cha luninga cha EATV.
“Tunafahamu watu wengi wangependa kuzishuhudia tuzo hizi zikitolewa kwa wanamuziki wetu lakini hawawezi kuwapo ukumbini, hivyo kituo cha EATV wataonyesha live tukio hilo,” alisema Kikuli.
Baadhi ya vipengele ambavyo wanamuziki wanachuana kuwania tuzo hizo ni pamoja na wimbo bora wakushirikiana, msanii bora anayechipukia, wimbo bora wenye vionjo vya asili, wimbo bora wa Afro Pop, msanii bora wa mwaka, mwanamuziki bora wa kike wa mwaka pamoja na mtayarishaji bora wa mwaka.
Vipengele vingine ni wimbo bora wa bendi wa mwaka, mtunzi bora wa mwaka wa bendi, mtunzi bora wa mwaka wa bongo fleva, wimbo bora wa RnB pamoja na wimbo bora Hip Hop wa mwaka.
Mpaka sasa bado wananchi wanaendelea kupiga kura kuchagua wasanii bora katika kila kipengele ambapo mwisho wa kupiga kura utakuwa ni muda mfupi kabla ya kutangazwa kwa washindi wa tuzo hizo.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved