Shein ataka makumbusho Zanzibar, Berlin kushirikiana

http://www.sautiyamnyonge.com/wp-content/uploads/2015/02/dr-shein.jpgRAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ametaka kuwepo ushirikiano kati ya makumbusho ya viumbehai ya mjini Berlin na Zanzibar ili kutoa fursa za kufanyika tafiti mbalimbali ya hazina ya viumbehai vilivyopo Zanzibar.
Akizungumza na uongozi wa makumbusho hayo mjini Berlin jana, Dk Shein alisema kuwa Zanzibar ina hazina kubwa ya viumbehai ambavyo havipatikani katika sehemu nyingine duniani lakini inashindwa kufanya tafiti za kina na kuziweka katika kumbukumbu kutokana na ukosefu wa wataalamu katika fani hiyo.
Kwa hivyo aliuambia uongozi huo kuwa Zanzibar iko tayari kuanzisha ushirikiano na makumbusho hayo kupitia Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale ya Zanzibar pamoja na Idara ya Historia na Akiolojia ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).
Katika mnasaba huo, Dk Shein ameukaribisha rasmi uongozi wa makumbusho hayo kutembelea Zanzibar, mwaliko ambao ulikubaliwa na uongozi huo.
Akitoa maelezo kwa Rais, Naibu Mkurugenzi wa makumbusho hayo anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa na Sera ya Sayansi, Dk Christoph Hauser alieleza kuwa atatuma timu ndogo ya wataalamu kutoka makumbusho hayo kwenda Zanzibar kuangalia namna kuanzisha ushirikiano na Idara ya Makumbusho ili kubadilishana uzoefu na kutoa mafunzo kwa kushirikiana na SUZA.
Aliongeza kuwa makumbusho yake iko tayari kuisaidia Zanzibar kuiunganisha na taasisi nyingine kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kufanya utafiti na kuziibua meli zilizozama baharini baina ya Visiwa vya Zanzibar na sehemu nyingine za mwambao wa Afrika Mashariki wakati Zanzibar ilipokuwa kituo kikuu cha Biashara kwa ajli ya kuzihifadhi.
Dk Christoph alifafanua kuwa taasisi yake bado inaendelea na utafiti wake nchini Tanzania kuhusu mabaki ya wanyama wa dinaso na wanategemea baada ya kumaliza kipindi cha utafiti kuandaa mkutano mkubwa wa kisayansi.
Aliongeza kuwa dhamira yao ni kuongeza hamasa kwa wananchi kuhusu taaluma hii, hivyo kuvutia vijana kujifunza na kupata wataalamu wengi wa kufanya kazi za utafiti na uhifadhi wa historia ya viumbehai.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved