Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alitangaza “kimya
kimya” nia ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM, jana alichukua fomu
kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho, akisema “ni Mungu pekee
ambaye anamjua Rais” wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Pinda, ambaye ameshikilia nafasi hiyo kwa takriban
miaka minane, hakutaka kutaja vipa umbele vyake kwa kuwa CCM haijatoa
Ilani ya Uchaguzi, lakini akasema katika kikao chake kifupi na waandishi
wa habari baada ya kuchukua fomu kuwa iwapo atapewa fursa ya kuongoza
nchi, “piga geuza nitahakikisha uchumi wa wanyonge unainuka”.
Pinda anakuwa kada wa 31 kuchukua fomu ya kuwania
kuteuliwa na chama chake, kupitishwa kuwania nafasi hiyo ya juu katika
siasa nchini.
CCM itahitimisha uchukuaji huo Julai 2 saa 10:00
jioni na makada wote waliochukua fomu hizo watatakiwa kuwa wamerudisha
fomu zilizojazwa na wadhamini kutoka mikoa 15 nchini.
Akizungumza jana mara baada ya kukabidhiwa fomu
hiyo, Pinda alisema ingawa kati ya wote waliochukua fomu kila mmoja
anataka apitishwe, Mungu pekee ndiye anayemjua Rais wa Tanzania.
“Mimi simjui, na wala wenzangu hawamjui na kila
mmoja anasema moyoni mwake kwamba atakuwa yeye, lakini ni Mungu tu ndiye
anayemjua,” alisema.
Pinda alisema hawezi kusema lolote kuhusu
vipaumbele vyake, hadi hapo Ilani ya Uchaguzi itakapopitishwa na Mkutano
Mkuu wa chama chake.
Hata hivyo, alisema ana uhakika hawezi kushindwa kutekeleza Ilani ya CCM.
“Ilani ndiyo itakayoeleza sera, maelezo na
mikakati yote, kwa hiyo sina cha kusema mpaka itakapopitishwa na
ikitokea nikateuliwa sitashindwa kuitekeleza na nalisema hili kwa
uhakika,” alisema Pinda mbele ya waandishi na wanachama wachache
waliohudhuria shughuli hiyo kwenye ukumbi wa ofisi za makao makuu ya CCM
mjini hapa.
Pinda alisema amefanya kazi na marais wa awamu zote kuanzia Serikali ya Mwalimu Nyerere na kwamba amejifunza mengi.
Alisema pia amekuwa Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka minane akiwa ndiye msimamizi mkuu wa utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Alisema Rais Jakaya Kikwete amefanya mambo mengi
ikiwemo kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo inayoishia mwaka 2025 dira
iliyoasisiwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
No comments:
Post a Comment