Waziri wa Fedha Saada Mkuya |
Akizungumza kwa kifupi jana kwenye Viwanja vya
Bunge mjini Dodoma, Mbatia ambaye hakutaka kuingia kwa undani akiahidi
mambo yote Jumatatu, alisema kuwa watawasilisha bajeti ikiwa na
vielelezo vyote, takwimu zilizofanyiwa kazi, bajeti ndogo lakini
inayokidhi na kugusa maisha ya Mtanzania.
Alisema kuwa bajeti ya Serikali imejaa mbwembwe,
lakini bajeti ya upinzani inalenga kwenye maeneo ya msingi, yanayomgusa
Mtanzania na yenye kueleza maisha nafuu ya Mtanzania. “Tumeangalia tozo
katika maeneo mbalimbali, tumeifanyia uchambuzi, inatekelezeka ni bajeti
rahisi,” alisema Mbatia ambaye ataiwasilisha kuanzia saa 10:00 jioni.
Baada ya bajeti kusomwa juzi, wabunge walipewa
siku tatu ili kupitia maeneo mbalimbali ya bajeti hiyo na kuwasilisha
hoja zao kwa ajili ya kuipitisha.
Akizungumza baada ya Mkuya kumaliza kuwasilisha
Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/16, Spika Anne Makinda ambaye hii ni
bajeti yake ya mwisho kuisimamia akiwa Spika, alisema: “Wale
mtakaoendelea na Bunge, muifanyie kazi bajeti hii, mhakikishe yote
yaliyopendekezwa mnayafanyia kazi.”
“Halafu mje tuijadili hapa. Tutaanza kuijadili
Jumatatu kwa siku saba mfululizo. Mje, hata kama mna homa ya uchaguzi,
siku saba haziwezi kuwavurugia mipango yenu. Tunataka mje tuijadili,
lakini bila matusi. Muungwana siku zote anashindana kwa hoja, mje na
hoja zenu, lakini si matusi,” alisema Spika Makinda ambaye tayari
ametangaza kutowania tena ubunge katika Jimbo la Njombe Kusini.
Kati ya waliotoa maoni yao ni Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye alisema bajeti hiyo haina nafuu
kwa Mtanzania masikini. “Haya ni maneno matamu ya kuwahadaa Watanzania
kwa kuweka vifungu vya kuwapa matumaini kwao,” alisema akisisitiza ni
bajeti ya kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Alisema kwamba kambi ya upinzani ilitoa maoni ya
kutaka kuanzishwa kwa mafao kwa wazee wote tangu bajeti ya mwaka
2012/2013. Hata hivyo, licha ya kutajwa tena wanafanya maandalizi ya
kuweza kutoa pensheni hiyo kwa wazee haitaweza kutekelezeka katika mwaka
wa fedha 2015/16.
Alisema haitaweza kutekelezeka kwa sababu hakuna
mpango wa kuileta sheria ya pensheni kwa wazee katika Bunge hili. “Hili
ni changa la macho kwa wazee hakuna atakayelipwa pensheni katika mwaka
ujao wa fedha,” alisema Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema).
Alisema, katika bajeti hii kuwapo ongezeko la kodi
na ushuru wa mafuta nchini wakati bei katika soko la dunia inapungua
kila siku kutaongeza gharama za maisha. “Watu wanaweza kufurahi sasa
miradi ya umeme vijijini itatekelezeka kwa kuwa fedha hiyo itaenda moja
kwa moja Rea (Wakala wa Umeme Vijijini) lakini katika mwaka uliopita,
ingawa fedha hizo ziliwekewa uzio, zilichotwa na kupelekwa katika
matumizi mengine,” alisema.
Alisema tatizo kubwa la nchi liko katika
utekelezaji wa mipango ya serikali. “Nusu ya mawaziri hawapo wakati
bajeti yao inasomwa bungeni. Kwa nini wabunge wao hawapo bungeni, sisi
wabunge wa kambi ya upinzani wote tulikuwa bungeni,” alisema.
TGNP waichana bajeti
No comments:
Post a Comment