Mkurugenzi wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Elias Chinamo akipelekwa rumande chini ya ulinzi wa polisi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana. Chinamo anatuhumiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa. Picha na Anthony Siame |
Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai
alidai wakati akisoma mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Renatus Rutta,
kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kati ya Juni 2011 na Februari
2013.
Swai alidai kuwa katika kipindi hicho mshtakiwa aliomba na kupokea rushwa ya zaidi ya Sh14.44 milioni.
Mwendesha Mashtaka huyo alidai kuwa Chinamo
alipokea rushwa ya Sh6.1 milioni kutoka kwa Suzana Nchala, fedha ambazo
alidai alizipokea kupitia akaunti yake yenye namba 0152237197600 iliyopo
tawi la benki ya CRDB la Holland.
Alidai kuwa alipokea fedha hizo kama faida ya
kumpa nafasi ya kuandaa semina mbalimbali na mikutano ya wizara hiyo,
kitu ambacho kipo kinyume na matakwa ya mwajiri wake.
Pia mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa Chinamo
alipokea Sh2.06 milioni kutoka kwa Fadhili Kilemile, fedha ambazo
zilipitishiwa kwenye akaunti hiyo kwa lengo la kumpa nafasi ya kuandaa
semina mbalimbali na mikutano ya wizara hiyo kinyume na matakwa ya
mwajiri wake.
Katika shtaka jingine, Chinamo anadaiwa kupokea
Sh3.28 milioni kutoka kwa Emmanuela Safari, Sh700,000 kutoka kwa Joseph
Bilango na Sh2.3 milioni kutoka kwa Anyitike Mwakitalima kupitia akaunti
ya CRDB na 019201018063 ya NBC, tawi la Kichwele.
Chinamo aliyakana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wake umekamilika.
Hakimu Rutta alimuachia huru mshtakiwa huyo baada
ya kukamilisha masharti ya kusaini dhamana ya Sh10 milioni pamoja na
kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya dhamana ya maneno yenye
thamani ya kiasi hicho cha fedha. Kesi imeahirishwa hadi Julai Mosi,
2015 atakaposomewa maelezo ya awali.
No comments:
Post a Comment