WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, amesema wingi wa makada wa CCM
wanaojitokeza kuchukua fomu za kugombea urais haumbabaishi, kwa kuwa
ndio mchakato wa demokrasia.
Hadi sasa kuna makada 31 waliochukua fomu za kugombea urais, akiwamo Lowassa mwenyewe.
Akizungumza katika mkutano wa kuwashukuru wana CCM waliomdhamini
wilayani Nzega jana, Lowassa alikitaka chama chake kutenda haki ili
kupata mgombea bora.
“Kumekuwa na wagombea wengi waliojitokeza kugombea. Huu ni mchezo wa
kupokezana vijiti, msiogope idadi ya wanaochukua fomu kwa kuwa ndiyo
demokrasia, ilimradi haki itendeke. Tuombe Mungu haki itendeke ili
tupate rais bora,” alisema Lowassa.
Aliwataka wanachama hao kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ili kumpigia kura zitakazomwezesha kuwa rais.
“Itakapofika tarehe 12 mwezi ujao, mkutano mkuu wa chama utaamua nani
anafaa kushika bendera. Tuwaombee wajumbe wa mkutano mkuu wachague mtu
mzuri. Kwa kanda hii ya ziwa, wallah nikipewa mambo yatakuwa vizuri,”
alisema Lowassa huku akishangiliwa na wana CCM hao.
Kwa upande mwingine mjumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho Wilaya ya
Nzega, Hussein Bashe, alimhakikishia Lowassa kuwa na kura 12 katika
mkutano wa CCM.
“Nakuhakikishia katika wilaya hii una kura 12 zitakazokuunga mkono
kwenye mkutano mkuu… kuna kura moja tu haieleweki, lakini ikifika Julai
12 itakuwa ya uhakika,” alisema Bashe, huku akishangiliwa na umati wa
wana CCM.
Bashe aliyasema hayo huku ikifahamika kuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Dk.
Khamis Kigwangalla, naye amechukua fomu ya kugombea urais kwa tiketi ya
CCM.
“Kumekuwa na maneno mengi, kila siku kuna santuri inatoka, lakini
nawahakikishia kuwa Lowassa yuko imara. Tumwombee tu ashinde,” aliongeza
Bashe.
Akimzungumzia Bashe, Lowassa aliwataka wananchi wa Nzega kumuunga mkono
kwa kuwa ndiye msaidizi wake wa karibu katika safari ya matumaini.
“Watu wamekuwa wakipita huku na huko kutafuta jimbo hili, lakini Bashe
hajaweza kwa sababu ni msaidizi wangu katika safari hii ya matumaini,”
alisema Lowassa.
Naye mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Arusha, Matthias Manga,
alimsifu Bashe akisema licha ya kuishi Dar es Salaam, amekuwa karibu na
wananchi wa Nzega.
Akitangaza idadi ya wana CCM waliomdhamini Lowassa katika Wilaya ya
Nzega, katibu wa Wilaya, Epimark Makwea, alisema wamejitokeza wanachama
3,816.
Akiwa mjini Tabora, Lowassa, aliyepata mapokezi makubwa, alisema anayajua matatizo ya mkoa huo, ukiwemo umasikini uliokithiri.
“Nayajua matatizo ya Tabora; kuna matatizo ya umasikini, reli ya kati na
tatizo la maji. Rais Mwinyi (Ali Hassan) alifanya yake, Rais Mkapa
(Benjamin) alifanya yake na Rais Kikwete (Jakaya) alifanya yake. Sisemi
kwamba walikosea, bali kila mtu alijaribu bahati yake. Ikimpendeza Mungu
nikifanikiwa nitaendesha mchakamchaka wa maendeleo,” alisema Lowassa.
Jumla ya wana CCM wa Tabora Mjini waliomdhamini Lowassa walifikia
9,516 ambapo kati yao, 45 ndio wamechukuliwa katika fomu ya udhamini.
Mkutano huo ulisheheni wazee wa CCM, akiwemo Mzee Nkumba, ambaye ni baba
yake Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba na Mbunge wa Urambo Mashariki,
Profesa Juma Kapuya na waziri wa zamani, Tatu Ntimizi.
No comments:
Post a Comment