MKUU wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya amesema kuwa tatizo la
utumikishwaji wa watoto nchini halitakwisha kama jamii haitakuwa tayari
kushiriki kikamilifu katika kupiga vita ajira za watoto.
Machibya alisema hayo mjini Kigoma katika maadhimisho ya Siku ya
Watoto Duniani yaliyoandaliwa na asasi ya Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji
(IRC) kupitia mradi wa WEKEZA ambao unatekelezwa mikoa ya Kigoma na
Tanga ukihusisha kuokoa watoto kwenye mazingira hatarishi.
Alisema kuwa wapo watoto ambao wamekuwa wakitumikishwa kwenye kazi za
mazingira magumu, ikiwemo kufanyishwa kazi za ndani, wakitumia muda
mwingi na kupata muda mchache wa kupumzika.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa wapo viongozi waandamizi wa serikali,
mashirika ya umma, taasisi za watu binafsi na watu binfasi ambao licha
ya kushiriki katika kampeni hizo, lakini wamekuwa wakishindwa kuchukua
hatua katika makazi yao ambapo vitendo hivyo vinafanyika.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za shirika la kazi duniani karibu
asilimia 80 ya watoto wanaotumikishwa duniani wapo kusini mwa jangwa la
Sahara barani Afrika ambapo hufanyishwa kazi kwenye maeneo ya vita,
migodi, mashamba na uvuvi.
Awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Costantine Samari, Mratibu wa
Mradi wa wekeza mkoa Kigoma alisema kuwa jumla ya watoto 5,041 wanaoishi
kwenye mazingira magumu na hatarishi wamenufaika na mradi huo kwa
kurudishwa shuleni na kupatiwa misaada mbalimbali.
No comments:
Post a Comment