KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye
amehimiza mshikamano nchini akihadharisha Katiba isiwe kigezo cha
kugawa wananchi na kusahaulisha kushughulikia matatizo yanayowakabili.
Nape alitoa rai hiyo juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara
uliofanyika mjini Ngara, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana mkoani Kagera. “Tuna sababu gani ya kugombana, tuna
sababu gani ya kutofautiana?
…tunatoana macho bure. Hakuna sababu ya kutoana macho, tunataka
kugawanyika bila sababu,” alisema Nape. Alisema wapo watu walidhani
kwamba katiba itakuwa njia fupi kwao kwenda Ikulu.
“Hupelekwi Ikulu na Katiba, unapelekwa Ikulu na kura za Watanzania,”
alisema Nape bila kubainisha watu hao. Hata hivyo, katika Bunge Maalumu
la Katiba, baadhi ya vyama vya upinzani, viliunda Umoja wa Katiba
(Ukawa) ambao umeendelezwa hadi sasa na kuamua kushirikiana katika
uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Nape alisema katika kuzunguka nchi nzima kupitia ziara hizo za Katibu
Mkuu, Kinana, wamebaini Watanzania wanaipenda CCM. Hali inayohakikishia
chama hicho kuendelea kuongoza nchi.
Akiendelea kusisitiza umoja wa kitaifa, Nape alisema wanaogombania
idadi ya serikali kuingizwa kwenye katiba, wengi wanaangalia maslahi
yao.
“Na ukiangalia sana, na hata hao wanaogombania mbili, tatu, nne kila
mmoja anatafuta ulaji wake. Mwenye mbili anafikiria kuwa hii mbili
nitapita, akiangalia akaona hakuna nafasi anasema tuongeze ya tatu na
mimi nitapata sehemu fulani,” alisema.
Alisema watu hao hawapambani juu ya maslahi ya nchi. “Mwito wangu
tutunze mshikamano,” alisema na kusisitiza wananchi kushikamana
nakutatua matatizo yanayowakabili. Alisema yako mambo mengi ya
kushughulikia kuliko kugombania katiba.
No comments:
Post a Comment