WAZIRI wa Uchukuzi, Samuel Sitta amefuta uteuzi wa wajumbe wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA) kuanzia
jana na kuteua wajumbe wengine wapya nane wanaounda bodi hiyo.
Uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa Kifungu Namba 6 Kifungu Kidogo
cha 2 (b) cha Sheria ya Bandari Namba 17 ya mwaka 2004, kinachompa
mamlaka ya kuvunja na kuteua wajumbe wa bodi.
Sitta alitangaza uteuzi huo jijini Tanga jana wakati wa ziara ya
kikazi katika Bandari ya Tanga na kisha kuzungumza na wafanyakazi katika
Uwanja wa Baraka bandarini hapo.
Alisisitiza kuwa mabadiliko hayo, yametokana na vitendo vya uonevu alivyokuta vikiendelea kufanywa ndani ya TPA.
Wajumbe wapya walioteuliwa ni pamoja na Mhadhiri wa Chuo cha Sheria
Tanzania, Dk Tulia Akson, Mhandisi wa Ujenzi, Norplan Consultants, Musa
Ally Nyamsingwa, Mtaalamu wa Manunuzi na Mjumbe wa Bodi ya Posta, Donata
Mugassa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa EWURA, Haruna Masebu.
Wengine ni Mhandisi wa Elektroniki wa Bodi ya Wahandisi Tanzania,
Gema Modu, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Francis
Michael, Mkurugenzi wa Mipango NSSF, Crescentius Magori na aliyekuwa
Mkurugenzi wa Masoko wa TPA, Flavian Kinunda.
“Uteuzi huu unatengua uteuzi wa wajumbe wa sasa wa bodi hiyo kuanzia
leo Juni 2, mwaka huu na lengo la uteuzi wa wajumbe hawa ni kuleta tija
na ufanisi wa utendaji kazi ndani ya wa Mamlaka”, alisema.
Uteuzi huo umefuta ule wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA,
uliofanywa Novemba 6, 2012 na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe uliofanywa kwa mujibu wa Kifungu cha 6(2) cha Sheria ya
Bandari na Kifungu 1(2(i)) cha jedwali la kwanza la Sheri ya Bandari ya
mwaka 2004.
Waliofutiwa ujumbe wa Bodi ni Dk Jabir Kuwe Bakari, John Ulanga,
Caroline Temu, Jaffer Machano, Dk Hildebrand Shayo, Said Salum Sauko,
Mhandisi Julius Mamiro na Asha Nasoro
No comments:
Post a Comment