Naibu waziri wa Elimu Na Mafunzo Ya Ufundi, Anne Kilango Malecela |
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango Malecela aliyasema hayo juzi bungeni wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Kilango Malecela alisema Mtaalamu Mwelekezi ameanza kazi jana na atamaliza Agosti Mosi, mwaka huu.
Alisema baada ya kazi hiyo, kutasaidia kupata mwongozo wa upangaji wa ada katika shule hizo binafsi na hasa baada ya wabunge wengi kulalamikia ada kubwa zinazotozwa na shule hizo binafsi nchini na kuiomba serikali iweke utaratibu maalumu wa udhibiti.
Naibu Waziri alisema pia ni marufuku kwa shule hizo binafsi kutoza ada kwa kutumia fedha za kigeni, isipokuwa kwa shule zile maalumu tu zikiwamo Shule za Kimataifa za Tanganyika (IST).
Aidha, Naibu Waziri alisifu ufaulu wa shule za sekondari za kata akisema zimekuwa zikifanya vizuri tangu zianzishwe na kwamba ubora wa elimu inayotolewa katika shule hizo umekuwa ukilingana na shule za binafsi.
Kwa upande wake, Waziri Dk Shukuru Kawambwa alisema serikali iko tayari kuanzisha Wakala badala ya Idara ya Ukaguzi na ameliwasilisha suala hilo kwa Waziri Mkuu kwa utekelezaji zaidi.
Aidha, alisema Muswada wa Sheria ya kuanzisha Tume ya Utumishi wa Walimu utawasilishwa katika Mkutano wa 20 wa Bunge unaoendelea sasa, kwani Bunge linatarajiwa kuongezewa siku 10 hadi Julai ili kukamilisha miswada mbalimbali.
Lilikuwa limalizike Juni 27, mwaka huu. Aliwatetea walimu kwa kazi nzuri na kubwa wanayofanya wakati mwingine katika mazingira magumu, na kuahidi kuwa serikali itahakikisha stahiki zao zinalipwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Kassim Majaliwa, alisisitiza kuwa malimbikizo ya madai ya walimu yatalipwa yote na tayari mengine yameanza kulipwa.
Majaliwa alisema baada ya uhakiki, zaidi ya Sh bilioni 25 zimelipwa na kwamba kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha 2014/15, madeni yote yatakuwa yamelipwa.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema Hazina itahakikisha fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu zinatoka kwa wakati. Pia aliipongeza Serikali ya Awamu ya Nne kwa kuongeza fedha hizo kutoka Sh bilioni tisa hadi kufikia Sh bilioni 350 kufikia sasa.
No comments:
Post a Comment