TFF yaagiza Simba, Singano wasaini mkataba mpya

http://globalpublishers.co.tz/wp-content/uploads/2015/03/MWE.png
Katibu Mkuu wa TFF, SelestineMwesigwa
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeamua kumaliza sakata la mkataba wa mchezaji Ramadhan Singano na klabu yake ya Simba kwa kuwaambia wasaini mkataba mpya.
Akizungumza na wandishi wa habari jana Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema kuwa TFF imekutana na Simba na Singano na kumaliza utata uliokuwepo kwenye mkataba huo.
Takriban mwezi sasa kumekuwa na mgogoro wa kimkataba kati ya Simba na Singano, mchezaji huyo akidai kuwa ameshamalizana na Simba kwani alisaini mkataba wa miaka miwili huku Simba ikisema mchezaji huyo bado halali yake mpaka Juni mwakani maana walisaini mkataba wa miaka mitatu.
Katika kikao cha jana kati ya pande hizo mbili na TFF, Simba iliwakishwa na mjumbe wake wa kamati ya Utendaji Collin Frich na Singano alikuwa ameambatana na Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji  (SPUTANZA) Musa Kisoky.
“TFF imeamua utata uliokuwepo kwenye mkataba kati ya Simba na mchezaji Ramadhan Singano umalizwe kwa kuingia mkataba mwingine  na pande zote mbili zimeridhia,” alisema Mwesigwa bila kueleza kwa kina.
Pia Mwesigwa alisema kuwa TFF ina mkataba mama ambao klabu na wachezaji wanatakiwa kuufuata kama mfano wakati wa kuingia mkataba na klabu na kuwataka wachezaji kuelewa mkataba kabla ya kutia saini.
Mwesigwa alisema kuwa wamewaita Simba na Singano ili kutapata suluhu na siyo kupata mshindi  bali kuhakikisha mchezaji na klabu kila mmoja anapata maslahi yake kwani tofauti ilikuwa kwenye mkataba kulingana na mkataba mama.
Naye Mwenyekiti wa SPUTANZA,  Kisoky alisema  amefurahi kupatikana suluhu kati Singano na Simba kupongeza TFF kwa kuingilia kati.
“Nimeridhika kwa matokeo ya mazungumzo ya pande zote mbili kwani tofauti ndogo tu imegundulika na Messi ni mchezaji halali wa Simba hadi hapo watakapoingia mkataba mwingine”, alisema.
Hata hivyo si Kisoky wala TFF waliokuwa tayari kuweka wazi tofauti iliyobainika kwenye mkataba huo ni ipi.
Pia alisema kuwa hakuna mahali ambapo mkataba ulikuwa umeghushiwa bali tofauti ilikuwa ndogo na amefurahi kwa upatanishi uliopatikana kwani.
Naye msemaji  wa Simba Haji Manara alisema yeye hana cha kuongeza kwenye maamuzi yao na kuwasisitiza wandishi kuheshimu maamuzi ya TFF.
“TFF ndio wenye mpira wao na wamefanya maamuzi ambayo tunatakiwa kuyaheshimu,”, alisema Manara huku akiingia kwenye gari .
Kwa upande wake mchezaji Singano alisema kuwa anamwachia Mungu huku akisisitiza kuwa yeye ni mchezaji huru huku uso wake ukionyesha kutoridhika na maamuzi.
“Mimi sina zaidi bali namwachia Mungu lakini natambua mimi ni mchezaji huru kwani mkataba niliokuwa nao unamalizika Julai,”, alisema Singano maarufu kama Messi.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved