UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema hadi kufikia Juni 16 utakuwa
umekamilisha usajili wa wachezaji watano wa kimataifa ili iweze
kuwatumia kwenye michuano ya Kombe la Kagame.
Akizungumza na gazeti hili Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha,
alisema wapo katika hatua nzuri kukamilisha usajili wa wachezaji hao na
baada ya Kamati ya Mashindano kupitisha idadi ya klabu kusajili
wachezaji 10 kutoka nje ya Tanzania watayaweka hadharani majina yao.
“Tuna uhakika Kamati ya mashindano itayapitisha mapendekezo yetu kwa
sababu bodi ya Ligi tayari imeridhia lengo letu ni kuongeza ushindani
kwenye ligi yetu lakini pia kuwapa changamoto wachezaji wazawa,”alisema
Tiboroha.
Katibu huyo alisema katika usajili wa nyota hao nguvu zao
wamezielekeza kwenye mataifa manne ambayo ni Zimbabwe,Ghana,Ivory
Coast,Nigeria na Sierra Leone.
Tiboroha alisema katika usajili huo mpya hakuna hata mchezaji ambaye
amewahi kucheza Ligi ya Tanzania na nyota hao wanatarajia kuanza
kuwasili nchini kuanzia mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya kukamilisha
mambo ya usajili.
“Tumekuwa makini katika usajili huo wa kimataifa kama tulivyofanya wa
hapa nyumbani kwa kuzingatia ugumu wa mashindano ambayo tunakwenda
kushiriki kuanzia msimu ujao na katika usajili huo hakuna mchezaji
yeyote aliyewahi kucheza ligi ya Tanzania,”alisema Tiboroha.
Katika hatua nyingine, jumla ya wachezaji saba walihudhuria mazoezi
ya kwanza jana asubuhi kwenye uwanja wa Karume chini ya kocha Mkuu Hans
van der Pluijm.
Wachezaji hao ni Rajabu Zahiri, Hussein Javu,Patto Ngonyani Said
Juma, kipa mpya Benedictor Tinoco aliyesajiliwa kutoka Kagera Sugar,
Geofrey Mwishuhuya na Lansana Kamara raia wa Sierra Leone.
Kocha Pluijm alisema amefurahishwa na nidhamu iliyooneshwa na
wachezaji hao kwa kuitikia mwito wa kuhudhuria mazoezi siku ya kwanza na
kusema ana imani hadi kukamilika kwa wiki hii kikosi chake kitakuwa
kimekamilika kwa idadi kubwa ya wachezaji kuanza mazoezi.
“Nawapongeza wachezaji waliofika leo (jana), ikiwa ni siku ya kwanza,
lengo langu nikuwa na kikosi imara ambacho kitatuwezesha kutetea
ubingwa wetu na hilo linawezekana kutokana na usajili tulioufanya
ukijumuisha na wachezaji wa kimataifa wanao tarajia kujiunga nasi siku
za karibuni,”alisema Pluijm.
No comments:
Post a Comment