KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Ramadhani Singano ‘Messi’ jana
alilakiwa kwa mbwembwe na mashabiki wa Yanga wakati alipofika makao
makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa ajili ya usuluhishi wa
suala la madai ya kughushiwa kwa mkataba wake.
Messi alifika uwanjani hapo akiwa sambamba na Mwenyekiti wa Sputanza,
Mussa Kisoky na kukutana na kundi kubwa la mashabiki wa Yanga waliofika
uwanjani hapo kwa ajili ya kutazama mazoezi ya timu yao yaliyoanza jana
kwenye uwanja wa Karume Dar es Salaam.
Baada ya mashabiki hao kumuona mchezaji huyo wakaanza kumshangilia
huku wakiimba Messi,Messi,Messi na wengine wakitaka kumvalisha jezi ya
Yanga lakini zoezi hilo lilishindikana kwa sababu alikuwa ndani ya gari.
Akizungumza kwa ufupi juu ya sakata hilo lililosababisha kuingia
kwenye chumba cha usuluhishi na viongozi wa timu yake, Messi alisema
anafurahi kuitwa sehemu hiyo kwa sababu haki yake itapatikana na kila
kitu kitakuwa wazi.
Baada ya kuzungumza maneno hayo mashabiki waliokuwa wamejazana
walianza kumshangilia tena mchezaji huyo wenye gari na kuwashukuru kwa
upendo waliomuonesha.
“Nawashukuru kwa upendo mlionionesha najua siyo kitu rahisi kwa
mashabiki wa Yanga kumshangilia mchezaji wa Simba na mimi nilijua
nitazomewa lakini sapoti mliyonipa imenipa faraja kwa hiyo
nawashukuru,”alisema Messi na kurudi ndani ya gari lililomleta TFF.
Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya TFF, ilizitaka pande zote
mbili yani Messi na uongozi wa klabu ya Simba kukaa pamoja jana, kwa
ajili ya kumaliza utata uliokuwepo juu ya sakata la kufojiwa kwa mkataba
wa mchezaji huyo.
Messi anasema mkataba wake wa kuichezea Simba unamalizika mwaka 2015
yaani mwishoni mwa msimu uliopita huku Kamati ya Usajili ya Simba chini
ya Mwenyekiti wake Zacharia Hans Poppe, ikidai mchezaji huyo mkataba
wake unamalizika mwishoni mwa msimu ujao.
No comments:
Post a Comment