Wabunge wahamasishwa kununua hati fungani

http://1.bp.blogspot.com/-NvO0-IJLSKo/VC1VPZbSbGI/AAAAAAADE0U/_1VjwiIsLE0/s1600/32.jpg
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Anne Makinda
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu amewahamasisha wabunge kununua hati fungani zinazotolewa na Benki Kuu kama njia ya kuhifadhia fedha zao na kupata faida.
Gavana Ndulu alitoa hamasa hiyo jana wakati akijibu hoja za wabunge, wakati wa semina iliyotolewa na BoT juu ya mwenendo wa thamani ya shilingi ya Tanzania mjini Dodoma.
Alisema mpaka sasa ni Watanzania wachache wanaonufaika na hati hizo, na baadhi yao ni wageni kutoka nje. “Wageni wanatazama, wananunua hati hizi fungani ama vipande vinavyouzwa na Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (UTTAMIS),” alisema.
Aliwashauri wabunge watakapolipwa mafao yao baada ya Bunge kumalizika wiki chache zijazo, wachangamkie fursa hizo za uwekezaji kwa kuwa una faida.
Alisema mtu anayewekeza pesa zake kwenye hati hizo, hasubiri hadi uwekezaji kuiva, miaka mitano au saba, bali kila baada ya miezi sita anapokea fedha.
Alisema mtu anayewekeza kwenye hati hizo ana uhakika wa fedha kuliko hata anayewekeza kwenye biashara ya kufuga kuku. Wabunge wengi walionekana kuhamasika na kuwa tayari kuwekeza kwenye hati hizo.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved