Shilingi kurejea kawaida yake

Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeanza kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha thamani ya Shilingi ya Tanzania, hatua ambazo imesema katika kipindi kifupi kijacho zitaifanya sarafu hiyo kuimarika.
Kasi ya kushuka kwa thamani ya Shilingi imekuwa kubwa ambapo takwimu za wiki hii zinaonesha kwamba Dola ya Marekani ilikuwa inabadilishwa kwa wastani wa zaidi ya Sh 2,000 za Tanzania kutoka Sh 1,629 Machi 2014.
Akiwasilisha mada kuhusu mwenendo wa thamani ya Shilingi katika semina liyoandaliwa na BoT kwa ajili ya wabunge mjini Dodoma jana, Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, alitaja moja ya hatua zilizochukuliwa kuwa ni kuongeza mauzo ya Dola katika Soko la Jumla la Fedha za Kigeni (IFEM).
Soko hilo la jumla (Interbank Foreign Exchange Market- IFEM) ndilo ambalo kwa sehemu kubwa linatoa mwelekeo wa kiwango cha ubadilishanaji wa fedha za kigeni.
Hatua nyingine alisema ni kupunguza ujazi wa fedha katika uchumi, ili kudhibiti miamala katika soko la fedha za kigeni. Hatua hiyo alisema inaenda sambamba na kupunguza uwezo wa mabenki kutumia zaidi fedha walizo nazo kufanya miamala katika IFEM ili kujinufaisha.
“Hatua hii ilianza kutekelezwa terehe 1 Juni, 2015,” alisema. Nyingine Gavana Ndulu alisema ni kudhibiti biashara za fedha za kigeni zisizoambatana na shughuli za kiuchumi, sambamba na kupunguza kiwango cha fedha za kigeni ambacho mabenki zinaruhusiwa kubaki nacho, ili zisitumie kujinufaisha kwa miamala ya fedha za kigeni.
Profesa Ndulu pia alisema kuongezeka kwa fedha za kigeni kutokana na kuanza kwa msimu wa utalii na mauzo ya bidhaa za kilimo nje kwenye nusu ya pili ya mwaka huu, kutasaidia pia kuimarisha Shilingi.
Lingine litakalosaidia kwa mujibu wa Gavana, ni kutolewa kwa fedha za wahisani na kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu.
*Sababu za kushuka
Akiorodhesha sababu za kushuka kwa thamani ya Shilingi yetu, Profesa Ndulu alisema ni pamoja na taharuki iliyoletwa na hisia za upungufu wa Dola katika soko, hali iliyosababisha ongezeko la mahitaji ya Dola hata kwa wale ambao hawana mahitaji ya msingi.
“Kadhalika, walio na Dola wanachelea kuziuza wakitazamia kuwa zitaendelea kupanda thamani huku wengine wakiamua kuzihifadhi kwenye mabenki ya biashara,” alisema.
Sababu zingine zilizosababisha kushuka kwa thamani ya Shilingi alisema ni kuimarika kwa Dola ya Marekani, mapato ya mauzo ya dhahabu nje kupungua kutokana na kushuka kwa bei ya madini hayo na kushuka na mauzo ya nje ya bidhaa za asilia hususan mazao ya kilimo.
Sababu zingine alisema ni ucheleweshwaji wa fedha kutoka kwa wahisani na mikopo ya kibiashara kutoka nje, kuingia kwenye msimu wa mapato kidogo ya utalii na bidhaa asilia, kuongezeka kwa malipo ya Serikali nje ya nchi (Foreign Government Obligations), kuongezeka kwa malipo ya wakandarasi na wasiwasi unaohusu uchaguzi.
Kuhusu wasiwasi wa uchaguzi, Gavana Ndulu alifafanua kwamba katika nchi nyingi, wakati wa kipindi cha uchaguzi baadhi ya wafanyabiashara wa kigeni huwa na tabia ya kuhamishia nje mali na fedha zao hadi baada ya uchaguzi kupita.
Athari za kushuka Akizungumzia madhara ya kushuka kwa shilingi yetu, Gavana huyo wa BoT alisema ni pamoja na kupanda kwa bei za bidhaa zinazoagizwa nje na hivyo kusababisha mfumko wa bei, kuongezeka mzigo wa kulipa madeni nje na wasiwasi wa uchumi kwenda mrama, hali inayoweza kupunguza uwekezaji.
Hata hivyo, alisema wapo wanaonufaika na kushuka kwa shilingi, ikiwa ni pamoja na wanaouza bidhaa na huduma nje kwani wanapata shilingi nyingi zaidi kwa dola moja wanayobadalisha.
Wengine wanaonufaika ni wale wanaopokea fedha kutoka kwa ndugu zao, walioko nje huku Serikali nayo ikiongeza mapato yatokanayo na kodi za bidhaa na huduma kutoka nje, yaani ushuru wa forodha.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved