WAFUGAJI wa Kanda ya Magharibi, wanakusudia kufanya maandamano kwenda
Ikulu kwa ajili ya kudai haki yao iwapo Rais Jakaya Kikwete hataitoa
kwa umma ripoti ya uchunguzi wa Operesheni Tokomeza.
Wamesema katika kuidai ripoti hiyo ya Tume ya Kijaji, pia watafunga
minada yote ya mifugo ya Kanda ya Magharibi inayoundwa na mikoa ya
Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa.
Kusudio hilo la kufanya maandamano lilitangazwa jana mjini Dodoma
mbele ya waandishi wa habari na Katibu wa Chama cha Wafugaji wa Kanda ya
Magharibi, Joseph Paroko.
“Ikifika Julai 30, Rais hajaweka hadharani taarifa ya Operesheni
Tokomeza, wafugaji wa Kanda ya Magharibi tutafanya maandamano makubwa
kwenda Ikulu kadai haki yetu,” alisema Paroko.
Alisema wafugaji wanataka taarifa hiyo iwekwe hadharani kwa sababu
hadi sasa waathirika wa Operesheni Tokomeza hawajui hatima yao na pia
wanaishi maisha magumu.
“Kwa mfano katika Kijiji cha Lumba, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora,
ng’ombe 2,537 walipigwa mnada kwa kutumia jina la Operesheni Tokomeza.
“Rais aliagiza operesheni hiyo isake majangili lakini badala yake
askari walikwenda hifadhi za misitu na kuwabambikizia kesi wafugaji,”
alisema Paroko.
Alisema katika operesheni hiyo, baadhi ya wafugaji walitapeliwa
ng’ombe na wengine waliuawa huku wakiwepo waliopata ulemavu wa kudumu
kwa kupigwa risasi na askari lakini hadi sasa hawajui hatima yao.
Sambamba na hilo, Poroko alisema wafugaji wanataka Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu, apeleke bungeni taarifa ya mapori ya hifadhi yaliyokosa sifa ya kuwa mapori ya akiba.
Alisema lengo la kuidai taarifa hiyo ni kulitaka Bunge litengue
sheria ya mapori hayo kuendelea kuwa hifadhi na badala yake wapewe
wafugaji kwa ajili ya kulishia mifugo yao.
No comments:
Post a Comment