Monica Mbega ajihakikishia kwenda Ikulu

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjjnQhpxgArMqJ6_9YM8DnIIiG6xoRUOQyzeyDvT0rDmbkwc7QU90_W2NVkntyV1gCoZM1uDJkKNld-Hz3DeAmElnmPjysPR8PuW7cQ7fQpFqMbCnR7lJQuaj1TCnFKH5L55XvkZumTQGmS/s640/DSC_0612.JPG
WAKATI mbio za makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaowania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais kupitia chama hicho zikiendelea kushika kasi, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Monica Mbega, jana ameingia mkoani hapa na kupata wadhamini 33.
Mwanamama huyo aliwataka Watanzania kutoaminishwa na mbwembwe za wagombea wenzake wanazofanya mikoani na kusema kuwa yeye ndiye rais wa awamu ya tano, huku akiwaomba Watanzania wamuunge mkono.
Mbega, ambaye alilazimika kusubiri wajumbe 30 wa kumdhamini kwa zaidi ya saa nne katika ofisi ya CCM Iringa Mjini, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya safari yake hiyo ya kutaka kwenda Ikulu na kudai kuwa amelazimika kuzuia viongozi wa CCM wilaya hiyo kutomuandalia mbwembwe zozote wala wapambe wa kumshangilia wakati wa safari ya kutafuta wadhamini.
Alisema anamtegemea Mungu zaidi katika safari yake hiyo ya kwenda Ikulu na ndiyo maana hakupenda kuweka makadirio ya gharama za safari nzima ya mchakato huo na wala hakutaka kuzunguka na wapambe zaidi ya dereva anayemuendesha.
“Naomba niwaelezeni wazi kuwa sina mgombea wa kumuunga mkono kati ya wote waliojitokeza zaidi ya 30, kwani naamini kuwa namba moja kati ya wote hao waliojitokeza ni Monica Ngenzi Mbega, ninasema hivyo kwa kuwa nchi ya sasa inahitaji mwanamke kuongoza, kwani mwenye kuweza kuvunja makundi ni mwanamke si mwanamume tena.
Alisema mwanamke ni mwepesi wa kusamehe, siyo mtu wa makundi, hivyo kama ndivyo ukitanguliza upendo makundi hayatakuwepo ya wenye visasi vya kutoka mwaka 2005.
“Ila siyo mimi ….mimi nimetanguliza upendo zaidi…mimi ni mama, nitaiunganisha nchi na changamoto inayomkabili rais wa awamu ya tano na kuiunganisha nchi na mimi ndiye pekee wa kuunganisha nchi hii.”
Kwa mujibu wa Mbega, iwapo chama chake kitamteua na Watanzania wakamchagua na kuingia Ikulu, wategemee Tanzania mpya yenye amani, upendo na mshikamano na uchumi bora kwa kila Mtanzania kuongeza pato binafsi .
Akielezea malengo yake, Mbega alianza kwa kunukuu kauli iliyopata kutolewa na Rais Kikwete kuwa misaada ambayo nchi inapata kutoka kwa wahisani mingine ina masharti magumu na ndiyo maana ya baadhi ya miradi kushindwa kukamilika kwa wakati, akisema iwapo yeye ataingia Ikulu atajaribu kukwepa misaada hiyo na kulijenga Taifa linalojitegemea lenyewe.
Pia alisema CCM bado ina nguvu zaidi katika Jimbo la Iringa Mjini na Tanzania kwa ujumla na iwapo suala la upendo likiwatangulia watia nia wote pale wanapokosa kuteuliwa kuungana kwa upendo kumuunga mkono aliyeteuliwa, suala la wapinzani kushinda litabaki kuwa ndoto.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved