Watanzania milioni 25 wapima Ukimwi


Waziri Wa Afya Na Ustawi Wa Jamii, Dk Seif Rashid
WATANZANIA milioni 25.4 wamejitokeza kupima Ukimwi kwa hiari, ikiashiria kwamba nusu ya Watanzania wamepima kujua hali yao kuhusu maambukizi ya Ukimwi.
Idadi hiyo ni ongezeko la watu milioni 4.9 waliopima kufikia Desemba 2013.
Takwimu hizo zimetolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake katika kikao cha 19 cha mkutano wa 20 wa Bunge.
Alisema hadi kufikia Desemba 2014, idadi ya watu waliopima virusi vya Ukimwi (VVU), walikuwa 25,468,564 na kufanya ongezeko la watu 4,999,323.
Kwa mujibu wa Waziri wanaopima VVU kwa hiyari imeongezeka kutoka watu 11,640 mwaka 2009 na kufikia 20,469,241 kwa mwaka 2013.
Alisema mafanikio hayo yametokana na kutekelezwa mpango mkakati wa lll wa sekta ya afya katika kupunguza maambukizi ya Ukimwi.
Alisema takwimu zilizopo zinaonesha kuwa kampeni imefanikiwa kuhamasisha wananchi na pia kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka asilimia 5.8 mwaka 2008 hadi 5.3 mwaka 2012 .
Alisema pamoja na kuendelea kutekeleza mpango mkakati huo wa tatu wa sekta ya afya wa kupambana na Ukimwi (2013-2017) kwa kutoa ushauri nasaha na upimaji wa VVU kwa hiari, wizara itaendelea kupanua huduma na upimaji kufikia ongezeko la watu 7,411,619 na kutoa dawa za ARV kwa waviu 880,681.
Aidha, alisema kwamba wizara yake imewezesha kliniki 109 zinazotoa ARV kwa wanawake wajawazito wenye VVU (Option B+) ziweze pia kutoa huduma za kupambana na Ukimwi kwa watoto wanaosihi na VVU.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved