KITENDAWILI cha Chama cha Wananchi (CUF) kuridhia hoja ya Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) kusimamisha mgombea mmoja wa nafasi ya urais
kwa upande wa vyama vya upinzani, kinatarajiwa kuteguliwa Jumamosi ya
wiki ijayo, ambapo Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa wa chama hicho litakaa
kujadili na kutoa uamuzi.
Hii ina maana kwamba, kama Baraza Kuu likipinga, itakuwa rasmi kwamba
ndoto za vyama vya upinzani kusimamisha mgombea mmoja zitafutika.
Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu Bara wa
CUF, Magdalena Sakaya alipokuwa akizungumzia ushiriki wao kwenye Ukawa
pamoja na kutohudhuria kwao juzi kwenye kikao cha Ukawa kujadili majimbo
ya uchaguzi na kumtaja mgombea nafasi ya urais kupitia kundi hilo.
Sakaya alisema CUF ni sehemu ya Ukawa na wanaendelea kushiriki kwenye
vikao vya kuafikiana maamuzi kwa hoja mbalimbali na kwamba hawajajitoa
kwenye Ukawa kama ambavyo baadhi ya mitandao na vyombo vya habari
vimeripoti. “Hatujajitoa Ukawa, sisi ni sehemu ya Ukawa na hatuwezi
kusaliti kitu tulichokiasisi wenyewe,” alisema Sakaya.
Na kuongeza, taharuki iliyopo mitaani kwamba CUF wamejitoa
inachangiwa na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo siku chache
zilizopita vimekuwa vikiripoti kwamba Ukawa imeshamteua mgombea nafasi
ya urais, jambo ambalo limezua taharuki kwa wanachama wa CUF, kwa kuwa
hawajatoa ridhaa hiyo.
Alisema kutokana na taharuki hiyo, wanachama wameingiwa na hofu ya
jambo hilo kwa kuwa hakuna ridhaa iliyoafikiwa na vikao vya maamuzi, na
kwamba hali hiyo imeifanya chama hicho kuitisha kikao cha Baraza Kuu la
Uongozi, chombo ambacho ndicho chenye maamuzi ya kutoa ridhaa hiyo.
“Baada ya kuona habari hizo kwenye baadhi ya vyombo vya habari na
mitandaoni, wanachama wetu wameingiwa na hofu ya ushirikishwaji na
tumeitisha Baraza Kuu la Uongozi litakutana Julai 25, mwaka huu,
tutajalidi na kutoa uamuzi wetu,” alisema Sakaya.
Kuhusu kushirikishwa kwao ndani ya Ukawa, Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya alisema kwa mfano kikao cha juzi
kilichofanyikia hoteli ya Colosseum, Dar es Salaam, walipata taarifa
baada ya kikao kuanza, hivyo walishindwa kuhudhuria kwa kuwa walikuwa
kwenye kikao cha dharura cha wanachama wao.
“Hizo taarifa za kikao cha Ukawa cha kumtangaza mgombea na
kuzungumzia majimbo ya uchaguzi mapya, mwenyekiti wetu alipata taarifa
mara baada ya kikao kuanza majira ya saa nne asubuhi, baada ya kuonekana
hayuko, hakuweza kuhudhuria kwa kuwa tulikuwa kwenye kikao kingine cha
wanachama wetu”, alisema Kambaya.
Aliongeza kuwa, kikao hicho cha jana taarifa za uwepo wake hazikuwa
wazi mapema na kwamba mwakilishi wao aliyehudhuria ni wa ngazi ya
wataalamu na sio ngazi ya viongozi wakuu, ambao ndio wenye maamuzi.
Kutokana na hali hiyo, alisema mkutano wa Julai 25 ndio utakaotoka na
maamuzi ya ama kukubali maridhiano ya Ukawa ya kusimamisha mgombea
mmoja au vinginevyo.
“Tunaomba tusubiri baraza la maamuzi likae, sisi tunafanya kazi kwa
kushirikisha wanachama wetu na baraza hilo, litakuja na maamuzi ya
masuala yote ya uchaguzi na mengineyo,” alisema Kambaya.
Juzi, katika kikao cha Ukawa kilichofanyika hoteli ya Colosseum
kilihudhuriwa na viongozi wa juu wa vyama vinavyounda kundi hilo,
isipokuwa kiongozi wa CUF, na kilipangwa kumtaja mgombea mmoja wa urais
kupitia kundi hilo atakayechuana na wagombea wengine, akiwemo wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli.
Hata hivyo katika kikao hicho kilichokaa hadi usiku saa tatu,
hakikumtaja mgombea wa nafasi hiyo na badala yake kilisema jina la
mgombea wanalo na kwamba watalitangaza ndani ya siku saba.
No comments:
Post a Comment