TIMU ya soka ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20, The
Tanzanites, jana ilianza vibaya harakati zake za kusaka tiketi ya
kucheza fainali za Kombe la Dunia baada ya kubugizwa bila huruma mabao
4-0 na Zambia katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Azam Complex
jijini Dar es Salaam.
Ni kipigo kizito kwa sasa Tanzanite inahitaji angalau ushindi wa
kuanzia mabao 5-0 wakati timu hizo zitakaporudiana nchini Zambia
baadaye.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ni miongoni
mwa watu walioshuhudia kipigo hicho cha kusikitisha kutoka kwa wenzao wa
Zambia The She-Polopolo.
Tanzanites inayofundishwa na mzalendo, Rogasian Kaijage ilizidiwa
karibu kila idara na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, walikuwa
tayari walishapigwa 3-0.
Mabao ya Shepolopolo yaliwekwa kimiani na Memory Phiri dakika ya nne,
Irene Lungu katika dakika ya 20 na Barbara Banda dakika ya 33.
Kipindi cha pili, Zambia iliingia uwanjani kwa nguvu na kupata bao la
nne huku The Tanzanite wakionekana kuimarika kidogo baada ya kupata
maelekezo kutoka kwa benchi la ufundi wakati wa mapumziko.
Wageni Zambia waliandika bao la nne dakika tano tangu kuanza kwa
kipindi cha pili lililofungwa kwa penalti na Marry Wilombe. Mwamuzi Refa
Batouli Ibrahim wa Sudan alitoa penalti hiyo baada ya Anastazia Anthony
kumfanyia madhambi mshambuliaji wa Zambia, Memory Phiri.
Kikosi cha Tanzania; Najjiat Abbas, Zuwena Aziz, Happiness Hezron,
Maimuna Hamisi, Anastazia Anthony, Donisia Daniel, Hamisa Athumani,
Neema Paulo, Asha Shaaban Hamza/ Janet Cloudy (dk 40), Shelider
Boniphace na Stumai Abdallah.
Zambia; Hezel Natasha Nali, Mary Wilombe/Osala Kaelo (dk 75),
Margaret Belemu, Martha Tembo, Mlika Limwanya, Lwendo Chisamu, Esther
Mukwasa, Irene Lungu, Grace Chanda, Barbara Banda na Memory Phiri/Agnes
Musesa (dk 83).
No comments:
Post a Comment