KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema wanachama
waliokihama chama hicho wamejivua nguo mbele za watu na kwamba wapinzani
wanaowachukua wanahangaika na mafuta machafu.
Aidha, amesema aliyekuwa Mbunge wa Segerea na Naibu Waziri wa Kazi na
Ajira, Dk Milton Mahanga, alikuwa anatafuta sababu za kuihama CCM na
anamtakia kila la heri, yeye na rafiki yake, Edward Lowassa.
Nape aliyasema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari
katika Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba, Dar es Salaam, alipotakiwa kueleza
kuhusu kuhama kwa Lowassa na Dk Mahanga ambao wote kwa nyakati tofauti
wamekimbilia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Lowassa alijitoa CCM wiki moja iliyopita baada ya kukwama uteuzi wa
CCM wa kuwa mgombea wake wa urais na kukimbilia Chadema ambako
anatarajiwa kuwa mgombea wake wa urais na kuungwa mkono na Umoja wa
Vyama vinne vya Upinzani (Ukawa).
Dk Mahanga naye alijitoa juzi baada ya kukwama katika kura za maoni
jimboni Segerea. “Wanahangaika na oil chafu. Hawa ni wale wale kama
ilivyokuwa Mrema (Augustino) mwaka 1995, akabebwa kiasi cha Mwalimu
Nyerere kusema mwacheni abebwa.
Hebu jiulizeni wanaona ubaya wanapotoka, lakini mambo yakiwanyookea
hawasemi, wakitoka ndio maneno mengi,” alisema Nape. Alisema kuondoka
kwa Lowassa na wengine wachache, si jambo la kwanza kutokea CCM, na pia
si la ajabu wala haliwezi kuwa la mwisho huku akimtuhumu Dk Mahanga kuwa
alikuwa akitafuta sababu ya kuondoka CCM.
Akizungumzia mchakato wake Mtama, Nape alisema kulifanyika juhudi
kubwa za mafisadi kuhakikisha anashindwa, lakini anashukuru ameshinda na
kwamba endapo atapitishwa na chama hicho kugombea ubunge, ana hakika
atashinda kwani ni mwadilifu na anayezingatia ya chama hicho ikiwamo
kupiga vita rushwa.
No comments:
Post a Comment