RAIS Jakaya Kikwete ameliagiza Baraza la Taifa la Usalama Barabarani,
kuanzisha mara moja mfumo wa ulipaji faini kwa njia ya Benki na
mitandao ya simu za mkononi ili kupunguza ushawishi wa vitendo vya
rushwa kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani nchini.
Pia, ameagiza kuanzishwa mfumo wa kuweka alama kwenye leseni za
madereva wanaokiuka sheria na kutumia njia hiyo kuwafungia, ikiwa ni
hatua mojawapo ya kudhibiti wimbi la ajali za barabarani hapa nchini.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo jana katika viwanja vya Tangamano
wakati alipokuwa akizindua Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani Kitaifa,
inayofanyika mkoani Tanga, ikiwa imebeba kaulimbiu inayosema ‘Endesha
Salama, Okoa Maisha’.
Alisema asilimia 56 ya ajali za barabarani, zinatokana na uzembe na
ukosefu wa umakini kwa madereva na kwamba hatua hiyo inasababisha vifo,
majeruhi na uharibifu wa mali na hata kuathiri ustawi wa Kaya na Uchumi
wa Taifa.
“Hivi mpaka sasa Baraza na Kikosi cha usalama barabarani
wanashindwaje kutumia mifumo ya kidigitali kwa nini mpaka leo hakuna
kamera barabarani? Kwanza ingesaidia kudhibiti ajali na uvunjaji wa
sheria, lakini hata vitendo vya rushwa ambavyo navyo vinachangia
ongezeko hili la wimbi wa ajali hapa nchini,” alisema Rais Kikwete.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2010 hadi 2014,
jumla ya watu 19,264 walipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani
na kwamba idadi ya ya waliokufa katika kipindi cha mwaka peke yake ni
watu 3,534 sawa na idadi ya wanaopeteza maisha kutokana na ugonjwa wa
malaria.
Kufuatia hatua hiyo, amelitaka baraza hilo kufanya mapendekezo ya
marekebisho ya sheria za usalama barabarani hasa pale penye mapungufu
ili kuweza kusaidia kudhibiti wimbi la ajali linalochangia upotevu wa
nguvu kazi ya Taifa.
“Kikosi cha usalama barabarani kiongeze kasi ya kudhibiti ajali za
barabarani na kuwachukulia hatua za kisheria Askari wanaojihusisha na
vitendo vya rushwa….lakini lisilale katika kutoa elimu ya sheria za
usalama barabarani hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari,”
alisisitiza Rais Kikwete.
Kwa upande Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama
Barabarani,Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Mohamed Mpinga alisema
lengo kuu la maadhimisho ya siku hiyo ni kuhamasisha matumizi salama ya
barabara pamoja na kuwakumbusha watumiaji namna rahisi ya kutumia
barabara ili kupunguza ajali zisizo za lazima.
“Tunapoadhimisha siku hii tunawakumbusha watumiaji kuwa ajenda kuu ya
Taifa ni mapambano dhidi ya ajali za barabarani, jambo ambalo linaweza
kuadhibitiwa kwa sababu ya uzembe na uvunjaji wa Sheria za
Barabarani”,alisema Kamanda Mpinga.
Hata hivyo, alisema katika maadhimisho hayo Baraza limejipanga
kufanya Mkutano Mkuu wa wadau utakaoshirikisha nchi wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki, sambamba na mafunzo kwa madereva 300 wa daladala
na walimu 200 wa shule za msingi kwa lengo la kujenga uelewa kuhusu
sheria za usalama barabarani.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Said Magalula alisema takwimu zinaonesha katika
kipindi cha mwezi Januari mpaka Juni mwaka huu, ajali za barabarani
zilikuwa 52 ambapo vifo vilikuwa 59 na majeruhi 68. Magalula alisema
mkoa huo kwa mwaka 2014 ulifanikiwa kuingia katika tano bora kati ya
mikoa ambayo imefanikiwa kudhibiti ajali za barabarani.
No comments:
Post a Comment