SIMBA ya Tanzania jana ilisherehekea vizuri siku yao (Simba Day),
baada ya kuifunga Club Sports Villa ya Uganda 1-0 katika mchezo
uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo ulikuwa mahsusi wa kuhitimisha wiki ya Simba Day, ambapo
mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Singida Mjini anayemaliza muda wake,
Mohamed Dewji.
Dewji hivi karibuni alitangaza kutogombea kiti hicho tena. Ushindi
huo ni mwanzo mzuri kwa kocha Muingereza Dylan Kerr ambaye hivi karibuni
alilalamikia ubutu wa safu yake ya ushambuliaji timu hiyo ilipokuwa
kambini Zanzibar, ambako ilicheza mechi kadhaa za kirafiki.
Bao hilo pekee lilifungwa na Awadhi Juma katika dakika ya 90 ya
mchezo huo baada ya kutokea piganikupige langoni mwa Club Sports Villa.
Simba iliuanza mchezo huo kwa kasi lakini jitihada zao za kusaka bao
zinakwamishwa na Hamisi Kiiza ambaye alishindwa kufunga bao la kuongoza
katika dakika ya 13 baada ya kupata nafasi nzuri lakini akachelewa
kufanya maamuzi na beki wa Club Sports Villa, Mbowa Paul akauokoa.
Villa wanajibu mapigo katika dakika ya 17 wakati Achema Robert
anakuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini anapaisha mpira nje ya
lango. Dakika ya 23 Simba iliendelea kukosa mabao wakati Mussa Mgosi
akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga, alipiga mpira nje. Dakika mbili
baadaye, Kiiza alipata mpira lakini kabla ya kulifia lango, mpira huo
unazuiwa na beki mmoja wa Villa.
Villa ilipata pigo baada ya mchezaji wao, Waibu Yeseni kutolewa kwa
kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumchezea Ibrahim Ajibu.
Dakika ya 55 Simba walikosa tena bao wakati Mgosi alipiga shuti
lililodakwa kirahisi na kipa wa Club Sports Villa, Odongo Steven, huku
Mohamed Hussein akipiga shuti nje ya 18 na kutoka nje ya lango.
Kikosi Simba: Vicent Angban, Ramadhani Kessy/Emiry Nimuboma, Mohamed
Hussein, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Justuce Majbva/Haji Nuhu, Said
Ndemla, Ibrahim ajibu/ Mwinyi Kazimoto,Hamisi Kiiza, Mussa Mgosi na
Peter Mwalyanzi/Simon Sserunkuma.
Aidha; Katika mchezo wa utangulizi ambao uliwahusisha viongozi wa
Simba na wasanii, Simba ilitamba kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0
katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja huohuo huku bao hilo pekee
likiwekwa kimiani na kocha wa timu hiyo, Kerr.
No comments:
Post a Comment