WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amesema hawezi kuhama Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na kuwataka waliohama baada ya kubwagwa kwenye kinyang’anyiro cha
kugombea urais, kujiuliza iwapo wataihama nchi wakishindwa kufanikisha
malengo yao huko walikohamia.
Pinda alisema hayo jana alipohutubia wakazi wa mikoa ya Nyanda za Juu
Kusini, alipokuwa akifunga maonesho ya wakulima ya Nanenane kwenye
viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Alisema wakati wa mchakato wa kura za maoni, kila mmoja alipokuwa
akizunguka mikoani kusaka wadhamini, alikuwa akiamini yeye ndiye
anayeweza kupita, lakini hatimaye wachache walivuka hatua ya kwanza na
wengine kuachwa nje na hatimaye mwisho akapatikana mmoja anayefaa zaidi.
Alisema haikuwa kosa kwa mmoja kati ya wagombea 38 waliorejesha fomu
kupewa nafasi hiyo, kwa kuwa chama kiliamini anafaa na hivyo
kinachopaswa kufanyika na makada wengine, ni kuendeleza chama ili
kishinde kwa kishindo.
“Tulijitokeza wengi kuchukua fomu, watatu wakashindwa kurejesha fomu,
wakawa wamejitoa wenyewe. Tulibaki thelathini na nane tuliorejesha fomu
na kati ya hao wapo waliopita na wengine wakawekwa pembeni. “Mimi pia
nikawekwa pembeni. Ninaamini kazi tuliyokwenda kuifanya tumeifanya
vizuri, tena vizuri sana. “Sasa hapa katikati nilikaa kimya kidogo, watu
wakaanza kusema kwenye mitandao… Oooh mbona mzee kimya! Au naye anataka
kuhamia kule. Sasa niseme nimeachwa huku kwa hiyo nifanyaje? Nihame
niende wapi? Hivi ukihama huku huko unakohamia ukishindwa utahamia wapi
tena? Au ndiyo utahama nchi? “Wana uhakika gani na huko wanakohamia?
Mbona nako kila siku tunasikia ya kusikia. Mivutano haiishi. Kila siku
tunaona mambo. Tutabanana hapahapa, kama ni kusahihishana
tutasahihishana humu humu,” alisema.
Hahami
Alisema hana mpango wowote wa kuacha chama hicho kwa kuwa amekulia
humo na manufaa mengi ameyapata kupitia chama hicho, ikiwemo madaraka ya
uwaziri mkuu kwa miaka nane.
Pinda alisema hataki kuwa miongoni mwa makada wachache wa chama hicho
waliohama na kusahau mema waliyofanyiwa, huku akisema watu hao
wametimiza usemi wa ‘Asiyeshukuru ni Kafiri’.
Aliwataka Watanzania kutodanganyika na viongozi wachache wenye uchu
wa madaraka, wanaoshawishi kutokubaliana na mambo mazuri yanayofanywa na
Serikali na badala yake wajiulize ni akina nani hao wanaotaka kuvuruga
Taifa?
Waziri Mkuu alisema CCM ina Ilani yenye sera nzuri, na ndicho chama
kinachopaswa kuaminiwa na Watanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao na
kuthibitisha kuwa anayo imani na sera ya CCM, hana mashaka kuwa chama
hicho kitapata ushindi mnono kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Waziri Mkuu huyo alipongeza jitihada zinazofanywa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi nchini (NEC) katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, ikiwemo
uandikishaji wapigakura ambao wamevuka malengo yaliyowekwa awali.
Alisema licha ya changamoto nyingi zilizoibuka tangu kuanza kwa
uandikishaji wapiga kura nchini kupitia mashine za Biometric Voters
Register (BVR), Tume imeandikisha zaidi ya wapiga kura milioni 24 na
imevuka malengo yaliyowekwa awali.
*Nyuki wavamia
Katika hatua nyingine, nusura shughuli ya kufunga maonesho ya
wakulima ya Nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ndani ya viwanja vya
John Mwakangale jijini Mbeya, iharibike baada ya kutokea kwa kundi la
nyuki waliovamia katika uwanja huo.
Nyuki hao walivamia eneo la Banda Kuu la mikutano ndani ya viwanja
vya John Mwakangale, wakati shamrashamra za kufunga maonesho hayo
zikiendelea.
Nyuki hao waliokuwa wakisafiri, walifika sehemu hiyo wakitokea upande
wa Kusini Mashariki mwa Uwanja na baada ya kufika hapo umati wa
wananchi ulipata wakati mgumu kwani wapo baadhi ya watu ambao walianza
kuhaha kwa kulala chini, huku wengine wakibaki wameduwaa wasijue la
kufanya.
Waandishi wa habari waliokuwa mashariki mwa jukwaa kuu, ni miongoni
mwa watu waliolazimika kuinama kwenye kichumba kidogo kusubiri kwa muda
mpaka nyuki hao walipoondoka.
Baada ya nyuki hao kupita, mwongozaji wa shughuli hiyo, Charles
Mwakipesile alimtania Pinda kuwa nyuki hao walipita kumsabahi rafiki
yao, kwa kuwa wanatambua kuwa amekuwa mstari wa mbele kupigania maisha
yao kutokana na faida kubwa walizo nazo kwa binadamu.
No comments:
Post a Comment