MATUMIZI ya dawa za kulevya nchini yameongezeka kwenye mikoa 12
nchini yakionesha dawa aina ya heroini na bangi zikiongoza kwa kutumiwa
zaidi.
Utafiti uliofanywa kwenye mikoa 12 nchini iliyopo pembezoni mwa
barabara kuu zinazounganisha miji au nchi nyingine, zikiwa kwenye hatari
zaidi ya wananchi wake kutumia dawa hizo.
Mikoa hiyo ni Mtwara, Dodoma, Morogoro, Pwani, Kilimanjaro, Tanga,
Arusha, Mwanza, Mbeya, Shinyanga, Geita na Kigoma. Wakiwasilisha matokeo
ya utafiti huo juzi Dar es Salaam, watafiti waliohusika kwenye kazi
hiyo, walisema kazi hiyo ilifanywa kati ya Julai 2013 na Agosti 2014
katika mikoa hiyo.
Mmoja wa watafiti hao, Moza Makumbuli alisema kutoka mikoa hiyo 12,
watumiaji wa dawa hizo wanapata shida kubaini aina ya dawa kati ya
heroini au kokeni, bali huita dawa hizo unga.
Katika mkoa wa Tanga, utafiti umebaini matumizi ya dawa za kulevya
yamesambaa kwenye miji midogo na vijijini nje ya mji kwenye maeneo ya
kandokando ya barabara ya Segera,Tanga.
Mkoani Mtwara, utafiti ulionesha watumiaji wa dawa kwa njia ya
kujidunga ni wachache ukilinganisha na wavutaji wa dawa hizo kwenye
Manispaa ya mkoa huo, lakini pia utafiti umeonesha Mji wa Masasi una
watumiaji wa dawa hizo.
No comments:
Post a Comment