TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Nkasi
mkoani Rukwa, inawashikilia wanachama 20 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
akiwemo diwani wa Viti Maalumu (CCM) aliyemaliza muda wake, wakituhumiwa
kutoa na kupokea rushwa.
Diwani huyo, Matrida Londezya ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa
Jumuiya ya Wanawake (UWT) wilaya ya Nkasi, anatuhumiwa kuwashawishi wana
CCM 20 kwa kuwapatia kiasi cha Sh 2,000 kila mmoja ili achaguliwe kuwa
diwani wa kata ya Nkomolo kwa tiketi ya CCM kwenye kura za maoni
zinazofanyika leo.
Kamanda wa Takukuru wilaya ya Nkasi, Samson Bishati alithibitisha
kukamatwa kwa watuhumiwa hao juzi saa 3:00 usiku wakiwa katika nyumba ya
mtu aliyetajwa kuwa Victor Sadala iliyopo katika eneo la kata ya
Nkomolo mjini Namanyere.
Sadala, ambaye anadaiwa kuwa wakala wa mgombea ni miongoni mwa
watuhumiwa 20 wanaoshikiliwa na taasisi hiyo ya kuzuia rushwa nchini.
“Nilikuwa na maofisa wenzangu watatu katika doria ya kuwatambua,
kuwabaini na kuwakamata wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa
katika mchakato wa kura za maoni za madiwani na wabunge wilayani Nkasi,”
alisema na kuongeza kuwa mtoa siri wao aliwataarifu kuwa kuna wanachama
wa CCM wapatao 20 wamekusanyika kwenye nyumba ya Sadala aliyewaita ili
kuwashawishi wampendekeze Londezya achaguliwe katika kura ya maoni.
Alisema kwa mujibu wa taarifa walizozipata ni kuwa mkusanyiko huo
ulilenga kugawana fedha zilizotolewa na mgombea huyo wa udiwani ili
wampatie upendeleo maalumu kwenye kura za maoni na baada ya kupokea
taarifa hiyo walikwenda moja kwa moja eneo la tukio na kukuta watu hao
na mgombea ambapo waliwakamata na wanawashikilia.
Kwa mujibu wa Bishati, walipofika eneo la tukio watuhumiwa waliwekwa
chini ya ulinzi ambapo mwenye nyumba alijaribu kukimbia kwa hofu, lakini
ilishindikana na sasa watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na uchunguzi
ukikamilika watafikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment