Mbowe alisema hayo jana katika Hoteli ya Ledger Plaza Bahari Beach kilipokuwa kinafanyika kikao cha Kamati Kuu ya Chadema jana.
“Siwezi kusema zaidi ya hapo,” alisema Mbowe alipoulizwa sababu za
kutokuwapo Dk Slaa katika vikao hivyo muhimu na kuongeza atatoa baadaye,
mrejesho wa kikao hicho.
Kauli hiyo ya Mbowe haikuondoa wingu zito lililotanda Chadema baada
ya kutoonekana hadharani kwa kiongozi huyo katika matukio manne muhimu
ya chama hicho kikuu cha upinzani, tangu waziri mkuu wa zamani, Edward
Lowassa ajiunge nacho.
Tofauti na Dk Slaa, Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika alionekana
jana kwa mara ya kwanza katika kikao hicho na kufuta uvumi uliokuwa
umesambaa kuwa alikuwa na mpango wa kuachana na Chadema kama inavyodaiwa
kwa Dk Slaa.
Viongozi hao walianza kutoonekana katika shughuli za chama tangu
Lowassa alipojiunga na Chadema Julai 28 na kukabidhiwa fomu ya kugombea
urais Julai 30 na juzi Agosti Mosi alipozirejesha.
Hata hivyo, viongozi waandamizi wa Chadema wamesema suala la
kutokuwapo kwa Dk Slaa halipaswi kukuzwa kwa kuwa ‘anafanya kazi
nyingine za chama.’
Alipoulizwa jana, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu
alisema: “Suala la kutokuwapo Dk Slaa ni kitu cha kawaida, anafanya kazi
nyingine huko, lakini pia kuna wasaidizi wake hapa ambao ni sisi
manaibu. Mlikuwa mnazungumzia Mnyika naye haonekani, si huyo. Hatuwezi
kuendelea kujibu ‘rumors’ (uzushi) wa kwenye mitandao… nyie subirini si
tupo mtaona kama yupo au la.”
Mnyika atinga kikaoni
Jana, Mnyika alionekana katika viwanja vya hoteli hiyo lakini alikataa kuzungumzia kwa undani suala hizo.
“Siwezi kuzungumza chochote,” alisema Mnyika na hata alipoulizwa ni
lini atawaeleza Watanzania juu ya kutoonekana kwake alisisitiza mara
tatu kuwa “Siwezi kuzungumza chochote.”
Chama hicho kinaendelea na mfululizo wa vikao vya vyombo vya juu
ambapo leo kinatarajia kutafanya kikao cha Baraza Kuu kabla ya Mkutano
Mkuu kesho kumpitisha mgombea wa urais kesho.
Kura za maoni Kibamba zaahirishwa
Mchakato wa kura za maoni wa kumpata mgombea wa ubunge wa chama hicho
katika Jimbo Kibamba utafanyika leo baada ya kuahirishwa juzi.
Kaimu Katibu wa Chadema Mkoa wa kichama Kinondoni, Rose Mushi alisema
kura hizo zitapigwa leo kuanzia saa nne asubuhi, Kimara Baruti. “Kila
kitu kinakwenda vizuri, nadhani kesho (leo), tutafanya mchakato huu wa
kura za maoni, kama kutakuwa mabadiliko nitakutaarifu,” alisema Mushi.
Awali, Mratibu wa Chadema Kanda Pwani, Casmir Mabina alisema: “Jana
(juzi), tulishindwa kufanya kwa sababu mmoja wa watia nia alikuwa
mgonjwa. Hakupata taarifa za mchakato huo, tukatumia demokrasia ya
kuahirisha.”
Mwenyekiti wa Jimbo la Ubungo, Boniface Jacob alisema kura za maoni
katika jimbo hilo (Kibamba) huenda zikafanyika leo baada ya kupokea
taarifa kutoka kanda. “Sisi kazi yetu ni kuratibu mchakato wa kura za
maoni ila maelekezo yote yanatoka juu, inawezekana ikiwa kesho (leo)
jioni sina uhakika,“ alisema Jacob.
Juzi, hali ya sintofahamu iliwakumbuka wajumbe na watia nia wa jimbo
hilo baada ya kufika kwenye ukumbi wa mikutano na kuambiwa kuwa mchakato
wa kura za maoni umeahirishwa kwa madai kuwa mmoja ya watia nia
hakupewa taarifa.
Hatua hiyo ilizua minong’ono miongoni wa wajumbe na watia nia ambao
waliokuwa wamejiandaa kwa mchakato huo wakidai kuna hujuma zinataka
kufanyika.
(CHANZO: MWANANCHI)
(CHANZO: MWANANCHI)
No comments:
Post a Comment