CHAMA Cha Mapinduzi Zanzibar kimesema hakitishwi wala kubabaishwa na
wingi wa wagombea wa vyama vya siasa wanaojitokeza kuchukua fomu za
urais wa Zanzibar kwani hiyo ndiyo demokrasia ya mfumo wa vyama vingi.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Kisiwandui mjini hapa, Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Vuai Ali Vuai alisema vyama vya siasa vitapimwa
kutokana na uwezo wake wa kusimamia na kutekeleza ilani ya uchaguzi
iliyojiwekea.
Alisema Chama Cha Mapinduzi kinajivunia na utekelezaji uliotukuka wa
Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010- 2015 ambayo imefanikiwa kwa asilimia 90
katika maeneo yote muhimu ikiwemo ustawi wa jamii, uchumi na sekta ya
kilimo.
“ Napenda kuweka bayana kwamba Chama Cha Mapinduzi hakibabaishwi wala
kutishika na utitiri wa wagombea wa vyama vya siasa walioibuka katika
kinyang'anyiro cha kuchukua fomu kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar
katika uchaguzi wa Oktoba 25......chama cha siasa kitapimwa na uwezo
wake wa kusimamia na kutekeleza ilani ya uchaguzi wake,” alisema.
Katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar tayari
jumla ya vyama 15 vimejitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi ya urais wa
Zanzibar ikiwa hiyo ni mara ya kwanza kuwepo kwa idadi kubwa ya vyama
vya siasa.
No comments:
Post a Comment