SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu madeni ya walimu kwa kusema
imeshalipa yote ya mwaka jana na kwa mwaka huu, orodha inaandaliwa.
Orodha kwa ajili ya madeni ya mwaka huu, inasubiriwa kutoka Ofisi ya
Waziri Mkuu (Tamisemi) kabla ya malipo kufanyika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile alisema jana
kwamba, wakati wa kulipa madeni ya mwaka jana, Wizara ya Fedha ilipokea
orodha kutoka Tamisemi ikionesha madeni ya Sh bilioni 19.6. Baada ya
kufanya uhakiki, walibaini madeni halali ni Sh bilioni 5.7 ambayo
walilipa yote.
Hali inayoonesha kuwa kuna watumishi hewa ambao waliingizwa katika
orodha hiyo ya madai. “Sababu za madai hayo kukataliwa ni pamoja na
kukosa vielelezo, madai yaliyokwishalipwa, madai yasiyo ya mishahara
kuwasilishwa kama mishahara, baadhi ya walimu kutotambuliwa na
Halmashauri husika na makosa ya ukokotoaji na uandishi,” alisema Dk
Likwelile.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa ufafanuzi huo jijini
Dar es Salaam, Likwelile alisema madai ya walimu yako mara mbili ambayo
ni mishahara pamoja na madai yasiyo ya mishahara.
Alisema mpaka sasa wizara haijapokea orodha ya madeni ya walimu kwa
mwaka huu, hivyo wataanza kuyashughulikia baada ya kuhakikisha walimu
wanapata fedha zao kwa wakati. Hata hivyo alisema upo umuhimu wa
Tamisemi kuandaa orodha ya madeni na kuyahakiki kutoa orodha ambayo
italipwa malipo halali.
Mkaguzi wa Ndani Mkuu, Mohammed Mtonga alisema kutokana na changamoto
zilizojitokeza wakati wa uhakiki ikiwemo kuongezwa kwa madai hewa,
idara yake inapendekeza kuwa halmashauri zilizowasilisha madai yenye
shaka, yasiyo halali au watumishi wasio na madai wawajibishwe kwa
kuwasilisha taarifa zisizo sahihi.
Mapendekezo mengine ni kuwa halmashauri hizo zihakikishe zinatenga
fedha kwa ajili ya kulipa madai halali ya watumishi wake, kuhakikisha
kuwepo kwa rejesta ya madai ya watumishi ambayo hayajalipwa na
yaliyolipwa.
No comments:
Post a Comment