MABOMU mawili yanayosadikiwa kuwa yalitegwa na watu wasiojulikana,
yamelipuka yenyewe na kuzua taharuki kubwa katika eneo la Michenzani
mjini hapa. Kamanda wa Kikosi cha Operesheni na Mafunzo cha Jeshi la
Polisi Zanzibar, Juma Yussuf alithibitisha jana kulipuka kwa mabomu
hayo.
Alisema uchunguzi zaidi un aendelea, kujua wahusika wa matukio hayo.
Juzi askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
walifanikiwa kutegua bomu moja, lililotengwa karibu na Kituo cha Polisi
cha Darajani bila ya kusababisha madhara.
Matukio hayo, mawili yamezua hofu na wasiwasi kuhusu amani na usalama
wa wananchi wa Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijatoa
tamko kuhusu matukio hayo pamoja na mustakabali wa hali ya kisiasa ya
Zanzibar, baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi
mkuu wa Oktoba 25.
Tamko la CCM
Wakati huo huo, Chama Cha Mapindizi (CCM) Zanzibar kimetoa tamko na
kuunga mkono uamuzi wa ZEC kufuta Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu
kutokana na ukiukwaji kwa taratibu za kisheria.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai akizungumza na
waandishi wa habari Ofisi Kuu Kisiwandui mjini hapa, alisema jana kuwa
uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, ulikuwa na dosari nyingi, ambazo
zilitosha kuufanya kuwa si huru na haki.
Alisema kitendo kilichofanywa na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi
ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kutangaza matokeo ni ukiukwaji wa
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Ibara ya 11 Kifungu 42 (5) na lengo
lake ni kuanzisha mgogoro wa kisiasa na vurugu.
“Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kinatoa tamko na kutaka uchaguzi mkuu
urudiwe kwa sababu ulijaa kasoro nyingi, kiasi ya kuufanya si tena
uchaguzi isipokuwa na uchafuzi,” alisema.
Kwa mfano, Vuai alisema mawakala wa CCM walinyimwa shahada za kuwepo
katika vituo vya kupigia kura, kitendo kilichodhihirisha kulikuwa na
lengo la kuvuruga na kupendelea chama kimoja ili kishinde uchaguzi huo.
Pia, alisema CCM inaishutumu ZEC, ikiwemo makamishna wake, kwamba
wanapaswa kulaumiwa kwa kushindwa kusimamia uchaguzi huo vizuri na
kujaribu kuingiza nchi katika machafuko. Vuai aliwataka wanachama wa CCM
kuwa watulivu na kuacha kuruhusu vijana wao, kujiingiza katika vurugu,
ambazo zimeitishwa na CUF.
Alisema matamshi yaliyotolewa na Maalim Seif, kwamba ataruhusu vijana
kuingia barabarani ni ya uchochezi, ambayo yanatakiwa kuchukuliwa hatua
na vyombo vya dola. Tangazo la ZEC Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar, Jecha Salim Jecha, wiki hii alitoa “Taarifa Kwa Umma ya Kufuta
Uchaguzi wa Zanzibar”.
Katika taarifa hiyo, Jecha Salim Jecha alisema “Mimi nikiwa
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi
huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa Sheria na taratibu za
uchaguzi. Hivyo, kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu
na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi
huu”
No comments:
Post a Comment