SERIKALI imesema tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini
linatokana na uchakavu na kuzidiwa kwa vituo vya kupoza umeme na
miundombinu ya usafirishaji na usambazaji nishati hiyo.
Katika kukabiliana na tatizo hilo Tanesco inachukua hatua za kujenga
mifumo ya njia kubwa za umeme wa msongo wa kilovoti 400 (Iringa-
Dodoma-Singida-Shinyanga), gridi ya Kaskazini Mashariki (Dar es Salaam,
Chalinze,Tanga –Arusha), ya Kaskazini Magharibi (Geita- Kagera –Katavi-
Kigoma- Rukwa na Mbeya) na Makambako- Songea wa kilovoti 220.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Dk Medard Kalemani wakati akijibu swali la Mbunge wa Magu,
Boniventure Kiswaga (CCM). Kiswaga alitaka kufahamu serikali
imejipangaje kukabiliana na tatizo la kukatika katika kwa umeme.
Pia mbunge huyo alitaka kufahamu, Je serikali itakamilisha lini
kupeleka umeme katika vijiji vya jimbo hilo ikizingatiwa mpaka sasa ni
asilimia 20 tu ya vijiji ndiyo vina umeme. Kalemani akijibu swali hilo,
alisema tatizo la kukatika kwa umeme linatokana na uchakavu na kuzidiwa
kwa miundombinu ya kupoza umeme pamoja na matukio ya kulipuka kwa
transfoma yanayosababishwa na radi hasa kipindi cha mvua pamoja na wizi
wa mafuta ya transfoma unaofanywa na wananchi wasio waaminifu.
Alisema Tanesco inakamilisha upanuzi wa usambazaji wa umeme katika
majiji makubwa ya Arusha, Dar es Salaam, na Mwanza ambapo kazi hizo
zitahusisha ujenzi wa njia mpya za umeme na kupanua vituo vya kupoza
umeme.
“Kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha KIA mkoani Kilimanjaro
kumeimarisha upatikanaji wa umeme maeneo ya Mirerani na Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA),” alisema Kalemani.
Pia vituo vya kupoza umeme katika jiji la Dar es Salaam vya Gongo la
Mboto, Kipawa, Mbagala, na Kurasini vitaunganishwa kwa njia ya sakiti
mzunguko kutoka Ubungo na Kinyerezi kuanzia Machi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment