Waziri wa Nishati ya Madini, Profesa Sospeter Muhongo amepinga uamuzi
wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kutumia zaidi ya Sh15 milioni
kununua transfoma katika kampuni binafsi badala ya kwenye Kiwanda cha
Tanalec Limited ambacho shirika hilo lina hisa zake.
Profesa
Muhongo alitoa uamuzi huo baada ya kutembelea kiwanda hicho jana
akiongozana na maofisa wa Tanesco, Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) na
maofisa wa wizara hiyo.
Katika ziara hiyo walibaini kuwa Tanesco hainunui transfoma katika kiwanda hicho.
“Kuacha
kununua Transfoma Tanalec hakuna sababu nyingine zaidi ya rushwa na
siyo kweli kuwa Sheria ya Manunuzi inawabana. Kama kweli inawazuia,
suala hili nitalifikisha kwa Rais (John Magufuli) na katika ngazi
nyingine za uamuzi,” alisema Profesa Muhongo.
Katika kiwanda
hicho, Tanesco inamiliki asilimia 20 ya hisa, Shirika la Maendeleo la
Taifa (NDC) asilimia 10 na Kampuni ya Transcentury ya Kenya inamiliki
asilimia 70.
Awali, kabla ya ubinafishaji Serikali ilikuwa ikimiliki asilimia 80 za hisa.
Kaimu
Meneja Mwandamizi wa Manunuzi wa Tanesco, Jasson Katule alisema shirika
hilo linashindwa kununua transfoma Tanalec kutokana na sheria kuwabana
kwa kuwa inawalazimisha kutangaza zabuni.
Alisema katika zabuni, Tanalec ilishindwa na kampuni za Quality Group na Intertrade ya India.
Kampuni
ya Quality Group itanunua transfoma za zaidi ya Dola 3 milioni za
Marekani na Intertrade imeshinda zabuni ya Dola5 milioni za Marekani.
Awali,
Meneja Mkuu wa Tanalec, Zahir Saleh alisema kiwanda hicho kwa sasa kina
uwezo wa kuzalisha transfoma 10,000, lakini kinazalisha 7,000 kutokana
na udogo wake.
Pia, alisema wanakabiliwa na changamoto za kukosa
soko la ndani huku wateja wakubwa yakiwa ni mashirika ya umeme ya
Kenya, Uganda na Zambia.