SERIKALI imesema katika mwaka ujao wa fedha itapunguza gharama za
upimaji ardhi kwa zaidi ya nusu ili kuwawezesha wanachi kupima maeneo
yao, hali ambayo inaonekana itapunguza migogoro ya ardhi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, William Lukuvi wakati wa ziara mkoani hapa kwa ajili ya kutatua
migogoro ya ardhi ambayo imedumu kwa miaka mingi.
Akizungumza na watendaji wa sekta mbalimbali wa mkoa wa Tabora,
Waziri Lukuvi alisema Wizara itapunguza kwa zaidi ya nusu, gharama za
upimaji ardhi ili kila mwananchi aweze kupima eneo lake na kupata hati
ya umiliki.
Lukuvi aliongeza kuwa serikali pia itaweza kukusanya kwa wingi kodi
ya pango la ardhi, hivyo kuongeza mapato ambayo yataisaidia serikali
katika kufanikisha shughuli za maendeleo.
Pamoja na kupunguza gharama hizo, Lukuvi aliwaonya maofisa ardhi
kuacha tabia ya kuendesha shughuli za serikali kwa kukiuka taratibu,
akitolea mfano wa maofisa hao kupima viwanja juu ya viwanja suala ambalo
limekuwa linaleta usumbufu mkubwa kwa wananchi.
“Maofisa ardhi lazima mfanye kazi kwa kuzingatia taratibu ili
kuepusha migogoro isiyo ya lazima ambayo inatokea miongoni mwa wananchi
na kuwasababisha kuichukia serikali yao,” alisema Lukuvi.
Alibainisha kwamba mtumishi yeyote wa idara hiyo atakayebainika
kukiuka taratibu atashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu na sheria za
kazi na zile za nchi.
No comments:
Post a Comment