Lowassa aanza safari yake

ALIYEKUWA Waziri Mkuu, Mbunge wa Monduli mkoani Arusha, Edward Lowassa, ametangaza nia ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili awe mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lowassa alitangaza nia hiyo katika uwanja wa Shekhe Amri Abeid, uliofurika watu waliokusanyika uwanjani hapo tangu saa 12 asubuhi wakimsubiri mtangaza nia huyo, aliyeingia uwanjani hapo kwa mbwembwe saa 9 mchana.
“Nina ari, shauku na uwezo wa kuongoza Tanzania. Hatumtafuti Rais tu, bali tunamtafuta Amiri Jeshi Mkuu na Mwenyekiti wa CCM. “Tunamtaka mzee mzoefu, mwenye ukomavu wa kisiasa aliyekaa ndani ya chama miaka ya kutosha na kukifahamu chama hiki,” alisema Lowassa.
Akizungumza katika hotuba iliyorushwa moja kwa moja na televisheni na redio kadhaa nchini, Lowassa alisema Watanzania wanahitaji mtu wa kuwaongoza kujenga Taifa imara.
Amesema Taifa hilo ni ambalo kila mwananchi wake anapaswa kuishi akiwa na uhakika wa usalama wa maisha yake, mali zake na mahitaji yake muhimu huku akijiridhisha kwamba leo yake ni bora kuliko jana yake.
Kwa mujibu wa Lowassa, Watanzania wanataka mabadiliko na wanaendelea kuamini kwamba CCM ina uwezo wa kusimamia mabadiliko hayo.
Hata hivyo, alikumbusha wosia wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alioutoa kwa wanaCCM mwaka 1995 wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Kwanza wa Mfumo wa Vyama Vingi kuwa: “Watanzania wasipopata mabadiliko ndani ya CCM, watayafuata nje ya CCM,” alinikuu hotuba hiyo na kusema ana uhakika na hana shaka CCM ina uwezo wa kuwapa Watanzania mabadiliko.
Lowassa aliweka wazi misingi mikuu ya utendaji wa Serikali atakayoiongoza, ikiwa CCM itampa ridhaa ya kugombea urais na wananchi wakimchagua kuwa Rais wa Awamu ya Tano.
Kwanza amesema ataongoza Serikali inayozingatia uwajibikaji, ambapo alidai kuwa Watanzania wanamfahamu yeye si mtu wa maneno, ni mtu wa vitendo.
Amesema anaamini kabisa kuwa hakuwezi kuwa na uongozi imara, utakaoweza kusimamia ujenzi wa Taifa imara, iwapo hakutakuwepo ujasiri wa kuwajibika.
Malengo yake Lowassa aliyekuwa akikatishwa hotuba zake kwa shangwe na kurudia rudia maneno kwa matakwa ya wananchi, alisema pamoja na kuwa Ilani ya CCM iko mwishoni ambayo itaelekeza Serikali inachopaswa kufanya, lakini mgombea pia anaruhusiwa kusema anachoamini.
Katika anayoyaamini, Lowassa alisema ataimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa kuimarisha misingi yake na kulinda misingi muhimu ya Muungano ya undugu wa damu na kihistoria, uliojengwa na waasisi Mwalimu Julius Nyerere na Shekhe Abeid Aman Karume pamoja na kuenzi Mapinduzi ya Zanzibar.
Lowassa aliahidi kupambana na hisia za udini na ukabila na kuimarisha siasa za uzalendo, huku akijenga uchumi wa kisasa na shirikishi utakaonufaisha Watanzania wote wa mijini na vijijini.
Mtangaza nia huyo, pia ameahidi kuondoa alichokiita sifa mbaya ya kuomba huku akisema kuwa anachukia sana umasikini, kwa kuwa kwa wingi wa rasilimali za Tanzania, ikiwemo mito na maziwa na ardhi kubwa, ataibadilisha nchi kuwa mkoba wa neema.
Katika ukuaji wa uchumi, Lowassa alisema atahakikisha ukuaji huo unaenda sambamba na upatikanaji wa haki za huduma muhimu kwa wananchi, ikiwemo huduma za afya na maji safi na salama.
Kwa mujibu wa Lowassa, marais waliotangulia kuanzia Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Nne, Benjamin Mkapa na Rais Jakaya Kikwete anayekaribia kumaliza muda wake, wamefanya kazi nzuri lakini kuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi.
Lowassa alisema katika fursa hiyo ya kufanya vizuri zaidi, ameazimia kuanzisha alichoita kuwa ni mchakamchaka wa maendeleo, huku akisema pia atapambana na rushwa kwa kuwa bila kupambana na rushwa, huduma na haki kwa wananchi hazitapatikana.
“Hatuwezi kujenga uchumi wa kisasa kama rushwa itatawala na Serikali haitatawala vizuri kama rushwa itaendelea kuwepo,” alisema.
Uwekezaji wa nje
Alisema Tanzania ya sasa imekuwa ni miongoni mwa nchi zinazovutia uwekezaji mkubwa katika sekta ya gesi ambayo inatajwa kwamba inaweza kuja kubadilisha kabisa maisha ya Watanzania.
Hata hivyo, alisema katika kipindi hicho kuelekea ujenzi wa uchumi wa kisasa, kimeibua hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi kwamba hawatanufaika na ukuaji huo wa uchumi na ugunduzi wa utajiri mkubwa wa gesi asilia.
Lowassa alisema vijana wanataka kuona ukuaji wa uchumi na ugunduzi wa utajiri huo unakwenda sambamba na uzalishaji wa ajira zenye maana, ili wakabiliane na changamoto za maisha yao.
Akizungumzia uongozi imara na Taifa imara, alisema Urais si kazi ya lelemama na inahitaji utashi na hata kabla ya kushawishiwa na wenzako, ni lazima kwanza wewe mwenyewe uamini na uwaaminishe wenzio kwamba unao uwezo wa kuwaongoza wananchi wenzako.
Mambo ya kujivunia
Alisema ana mambo ya kujivunia ikiwa ni pamoja na kushiriki katika vita ya Kagera ya kumng’oa Iddi Amini akiwa askari wa mstari wa mbele na kutokana na rekodi hiyo, anaamini kuwa ana sifa za kuwaongoza Watanzania katika zama mpya za ujenzi wa Taifa la kisasa.
Mbali ya Taifa la kisasa pia lenye watu wazalendo, walioshikamana na lenye uchumi imara unaomnufaisha kila Mtanzania, amesema kuwa anao uwezo wa kuwapa Watanzania uongozi imara kwa ajili ya ujenzi wa Taifa imara na hiyo ndio safari ya matumaini.
Kingunge
Naye mwanasiasa mzoefu, Kingunge Ngombale Mwiru alisema kuwa Waswahili walinena kuwa ‘’mzigo mzito mpe Mnyamwezi’’ na yeye anasema ‘’mzigo mzito mpe Lowassa.” Kingunge alisema Lowassa ameanzisha safari ya kuelekea Ikulu hivyo wote na kwa niaba ya wazee wenzake watamuunga mkono katika safari hiyo ya matumaini bila wasiwasi wowote.
Alisema nchi inahitaji kiongozi bora mchapakazi na mwenye uthubutu hivyo sifa zote hizo anazo Lowassa na aliwataka wakazi wa Arusha na nje ya Arusha kumuunga mkono mgombea huyo wa CCM.
Alisema asilimia 30 ya Watanzania wana umasikini sugu wa kupindukia na hakuna mabadiliko katika awamu zote hivyo Lowassa anahitajika apambane na hali hiyo na ikiwezekana amalize ama apunguze.
‘’Ninamshukuru na kumpongeza Lowassa kwa kutangaza nia yake ya kuelekea Ikulu hivyo anapaswa kuungwa mkono kwa hali na mali.’’‘’Huu umati uliokuja hapa kutoka kila kona ya nchi kuja kumsikiliza Lowassa sijawahi kuona kwani mara ya mwisho niliuona wakati tunamsubiri Mwalimu Nyerere arudi kutoka Umoja wa Mataifa kuleta Uhuru,” alidai.
Wanaofuata
Baada ya Lowassa jana kutangaza nia, leo itakuwa zamu ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wassira atakayetangazia nia jijini Mwanza kwenye Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Aidha Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba naye atatangazia nia yake mkoani Dodoma kwenye Chuo cha Maendeleo ya Mipango, eneo la Msalato.
Wanachama wengine wa CCM watachukua fomu wiki ijayo kuanzia kesho akiwamo mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Charles Makongoro Nyerere, William Ngeleja, Profesa Mark Mwandosya na Bernard Membe.
Mbali ya hao, orodha inayotajwa inawahusisha Lazaro Nyalandu, Amina Salum Ali, Dk Hamis Kigwangalla, Dk Titus Kamani, Shamsi Vuai Nahodha, Dk Emmanuel Nchimbi, January Makamba, Frederick Sumaye, Profesa Sospeter Muhongo na Dk Asha-Rose Migiro.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved