Wabunge Afrika Mashariki wawe bora
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe amependekeza mfumo wa kupata wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Tanzania ubadilishwe.
Waziri huyo aliyasema hayo juzi alipokuwa akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa Mwaka wa Fedha wa 2015/2016 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, ipo haja ya kubadili mfumo wa kupata wabunge hao kutoka Tanzania, hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa Bunge la Afrika Mashariki ndicho chombo kikuu cha kutunga sheria za jumuiya.
Waziri anafafanua zaidi kuwa sheria hizo kwa mujibu wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya, zinapewa nguvu juu ya sheria za nchi wanachama katika masuala ya utekelezaji wa mkataba huo.
Anasema wajumbe wa bunge hilo wanaruhusiwa kimkataba kuwasilisha hoja na miswada binafsi bungeni kwa majadiliano na uamuzi, lakini fursa hiyo imetumiwa vizuri na wawakilishi wa baadhi ya nchi wanachama kwa maslahi mapana ya nchi zao kuliko ilivyo kwa wawakilishi wa Tanzania.
Mbali ya hilo Waziri Mwakyembe anasema kutokana na hali hiyo kuna umuhimu wa Watanzania kuacha mfumo wa sasa wa kuwapata wabunge hao na kuangalia mfumo utakaopeleka watu watakaokuwa wazalendo na watakaotetea maslahi ya Tanzania, katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa dhati kabisa tunaungana na Waziri Mwakyembe katika kupendekeza mfumo unaotumika sasa katika kuwapata wabunge hao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ubadilishwe haraka iwezekanavyo kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
Kama alivyosema Waziri na kama inavyofahamika, utaratibu wa kuwapata wabunge wa Afrika Mashariki umekuwa hauna tija kwa maslahi ya Taifa letu na kwa muda mrefu umekuwa ukilalamikiwa kutawaliwa na rushwa na ushabiki zaidi kuliko kuangalia vigezo vya utaalamu na elimu kwa wahusika.
Hatua ya kukosekana kwa sifa kwa wabunge wanaochaguliwa kwenda kuliwakilisha Taifa kwenye jumuiya hii muhimu katika ukanda wa Afrika Mashariki ni hatari kwa mustakabali wa Taifa letu kwani kuna uwezekano mkubwa wa maslahi ya Tanzania kutozingatiwa ipasavyo.
Kama inavyofahamika, jumuiya za kikanda ni maeneo yanayopewa msukumo mkubwa katika diplomasia ya dunia ya leo, ambapo mataifa yote duniani yamekuwa yakipeleka nguvu katika kuvijengea uwezo vyombo vyake vya uwakilishi katika kanda zao kufahamu namna ya kushindana na kutetea maslahi ya mataifa yao ndani ya kanda zao.
Kutokana na changamoto hii ya wabunge wetu wa Afrika Mashariki kuchaguliwa kwa rushwa bila kuwa na sifa ni vigumu kuwapata wawakilishi wenye uwezo na uelewa mpana wa kufahamu namna ya kujenga hoja katika Dunia ya leo yenye kuelemea zaidi kwenye ushawishi wa Diplomasia ya Uchumi jambo ambalo ni la hatari kwa Taifa letu.
Ni lazima sasa suala la upatikanaji wa wabunge wa Afrika Mashariki, likatazamwa upya ili wabunge watakaochaguliwa wawe na uwezo mkubwa wa kujenga hoja mbele ya wabunge wengine kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya, nchi ambazo zinaonekana wazi zimepania kutumia fursa za ndani ya jumuiya kutetea maslahi ya mataifa yao.
Kwetu sisi tunaona kwamba bado hatujachelewa. Bado tunao muda wa kurekebisha kasoro zinazojitokeza katika kuwateua wawakilishi wetu kwenye jumuiya za kikanda ili kuhakikisha kuwa tunapata maslahi kama ambavyo malengo yetu ya kujiunga yanavyojieleza
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment