KLABU ya Yanga inajiandaa na maisha ya bila mfungaji bora wa Ligi Kuu
ya Soka ya Tanzania Bara Simon Msuva ambaye alifanya majaribio ya
kujiunga na klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Kocha Msaidizi wa Yanga Charles Mkwasa aliliambia gazeti hili jana
kuwa Msuva atajiunga na klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini na wao
kama makocha lazima watatafuta mtu wa kuziba nafasi yake.
Kama Msuva ataondoka Yanga atakuwa mchezaji wa pili baada ya Mrisho
Ngassa kutimkia kwenye klabu ya Free State ya Afrika Kusini na benchi la
ufundi la Yanga likamsajili winga Deus Kaseke kuziba nafasi ya winga
huyo wa kimataifa wa Tanzania.
“Kama hivyo Msuva anaondoka lazima tutasajili mtu kuziba nafasi yake,
hivyo kila usajili tutakaofanya utalenga katika kuangalia mapungufu ya
timu yetu,” alisema Mkwasa.
Alipoulizwa na mwandishi wa gazeti hili kama ofa ya kumtaka mfumania
nyavu huyo ambaye alienda kufanya majaribio Afrika Kusini mwezi uliopita
ishawafikia Mkwasa alisema kuwa kwa kuwa alienda kufanya majaribio
lolote linaweza kutokea na wao lazima wajiandae kwa hilo.
Tayari benchi la ufundi kwa kushirikiana na Kamati ya Usajili ya
klabu hiyo ishawapa mikataba wachezaji Kaseke kutoka Mbeya City, Haji
Mwinyi kutoka KMKM ya Zanzibar na kipa chipukizi Benedict Tinocco kutoka
Kagera Sugar.
No comments:
Post a Comment