MAOFISA watano wa Serikali, wanatarajiwa kupandishwa kizimbani hivi
karibuni, kutokana na kashfa ya uagizaji wa mabehewa 274 kutoka India,
huku wengine wakitarajiwa kuchukuliwa hatua za kiutawala.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ameliambia Bunge jana kuwa Kamati
Maalumu iliyoundwa na wizara yake, imemaliza kazi na kumkabidhi ripoti
hiyo. “Hii ndio ripoti ya Kamati (akionesha kwa wabunge).
Wamenikabidhi ripoti juzi na iliundwa na watu wa Ofisi ya CAG
(Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali), Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) na
wahandisi,” alisema Sitta.
Alikuwa akifanya majumuisho ya hoja za wabunge kuhusu makadirio ya
bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2015/16, ambayo aliyawasilisha bungeni
jana asubuhi na kupitishwa na Bunge baadaye mchana.
Waziri huyo mkongwe alisema kamati hiyo ilienda hadi Calcutta, India
ambako mabehewa hayo 274 yalitengenezwa na kwa mujibu wake, mabehewa
hayo si chakavu, kama ilivyodaiwa awali.
Hata hivyo alisema “kuna makosa mawili hapa ambayo ni uzembe wa pande
mbili, waagizaji na watengenezaji. Kuna tatizo katika specification
(vipimo). “Hapa kuna majina ya watu wote waliohusika katika suala hili.
Watano tunawapeleka mahakamani, wengine tutawachukulia hatua za
kiutawala.” Aidha, aliweka bayana kuwa katika maofisa hao watano
watakaopelekwa mahakamani, wawili ni wanachama wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA).
Mbunge huyo wa Urambo Mashariki alilazimika kusema hayo baada ya
Kambi Rasmi ya Upinzani kudai kuwa Serikali imekithiri kwa ufisadi,
akisema ufisadi unafanywa na watendaji.
“Kuweni makini sana mnapozungumzia suala la ufisadi na wizi, hili si
suala jepesi. Ufisadi si suala la kubadili sura. Ufisadi ni njama za
watendaji na halina vyama.
“Nataka kuwaambia kuwa kwenye hii shughuli ya reli (kashfa ya
mabehewa), wapo watendaji wawili ambao ni wanachama wa Chadema. Ndio,
subirini tukiwapeleka,” alisema Sitta na kuihoji Chadema kuwa inasema
CCM kuna ufisadi je, inapomchukua mwanachama wa CCM, ufisadi unabadilika
anapoingia kwao?
Akifafanua sakata hilo, alisema katika suala la vipimo limeonekana
kuwa havikuzingatiwa kwani mabehewa hayana milimita za kutosha, hivyo
kuwapo na matatizo katika ukataji wake na wakati treni ikiwa safarini.
Alisema kutokana na hilo, mtengenezaji ameitwa na yuko katika
karakana nchini, ambapo kwa gharama zake anafanya marekebisho katika
mabehewa hayo yaliyoanza kutoa huduma katika treni mwezi uliopita.
Aidha, Sitta alisema si kweli kuwa hasara iliyopatikana ni Sh bilioni
200, bali ni Sh bilioni 12 na wote waliohusika watachukuliwa hatua
stahili. “Pia tumemwomba Mwanasheria Mkuu ili sehemu ya hasara hii
ibebwe na mtengenezaji na nyingine itabebwa na Serikali kutokana na
uzembe uliofanyika,” alisema Sitta.
Waziri huyo alilazimika kusema hayo baada ya baadhi ya wabunge kumjia
juu, wakitaka eleze kwa kina nini kimetokea uagizaji huo wa mabehewa
uliofanywa wakati wa utawala wa Waziri Dk Harrison Mwakyembe.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alisema
ufisadi huo ni zaidi ya kashfa ya Richmond na kuwa Waziri husika, Katibu
Mkuu na Katibu Mkuu Hazina, walipaswa kujiuzulu mara moja.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema kashfa hiyo
inaendeleza ufisadi uliotamalaki serikalini na kumtaka Sitta aweke
bayana hatua alizochukua.
Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi (Chadema), Haroub Mohamed Shamis
(CUF), pia walizungumzia hilo. Aidha, Sitta aliahidi kufuatilia ripoti
ya CAG kuhusu uuzwaji wa nyumba za Mamlaka a Reli ya Tanzania na Zambia
(TAZARA) jijini Dar es Salaam na Mbeya.
Mapema mwezi uliopita, Sitta alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji
wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Kipallo Kisamfu na wengine wanne, ili
kupisha uchunguzi wa kashfa ya uingizaji wa mabehewa feki ya mizigo.
Wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Mitandao, Ngosomwile
Ngosomiles, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa, Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper
Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand Soka.
Alisema mabehewa mabovu yaliingizwa nchini mwaka jana kupitia
kandarasi ya Kampuni ya M/S Hindustan Engineering and Industrial Limited
ya India, ambayo ililipiwa asilimia 100 ya gharama zote ambazo ni Sh
bilioni 230.
Alitoa wiki tatu kuanzia Aprili 20, mwaka huu kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wa sakata hilo.
No comments:
Post a Comment