Waandishi wa habari wana kera kuchanganya lugha


NILIWAHI kusema hapa siku za nyuma kuwa bado ninavutiwa na nitaendelea kuvutiwa na watangazaji wa vipindi vya michezo na watangazaji wa mpira wa zamani kuliko wa kizazi hiki, ambacho bado ninaweza kusema kimeshindwa kukonga nyoyo za wadau.
Kuna tatizo kubwa kwenye kuandaa vipindi vya michezo kwenye radio mbali mbali na luninga hapa nchini pamoja na kutangaza matangazo ya moja kwa moja ya mpira wa miguu ingawa teknolojia inakibeba kizazi hiki, lakini tumeshindwa kutumia vyema nafasi hiyo.
Zamani hakukuwa na runinga ila ulikuwa ukisikiliza mpira wa miguu kupitia Radio Tanzania ulikuwa unadhani kama uko uwanjani vile au unautazama moja kwa moja kwenye runinga kumbe ulikuwa unasikiliza kwenye redio. Haya tuachane na hayo, leo hii ninataka kuzungumzia suala moja tu la lugha kwa watangazaji wetu wa mpira na vipindi vya michezo wa kizazi hiki, pamoja na watu wapya kabisa kwenye utangazaji wa mpira na vipindi vya michezo.
Hawa wenyewe wanawaita wachambuzi. Yaani wenyewe hawawezi kutangaza au kuchambua mchezo kwa lugha moja tu ya Kiswahili, lazima wataingiza kiingereza katikati hadi inakera tena sio kidogo na mbaya zaidi wakiongea hicho kiingereza chao hawatafsiri hata kidogo na wakati mwingine utamsikia huyo mtangazaji au mchambuzi akiongea sentesi nzima ya kiingereza na baadaye anaendelea tena kwa Kiswahili, hapo ninakosa jibu kabisa.
Sasa ninajiuliza hiyo redio au runinga anayofanyia kazi imesajiliwa kurusha matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili ila yeye anajimwaga tu kwa kiingereza, kwa nini hasa?
Na wahusika wapo wapi au nao wanaridhishwa na hali hiyo. Miaka ya nyuma watangazaji walifanya kazi vizuri, tena sana na walijijenga kwa kupitia lugha hiyo hiyo ya Kiswahili na hawakuwa na mbwembwe kama zenu za kuingiza lugha ngeni kwenye matangazo yenu, inakera tena sio kidogo.
Mtu anayefanya hivyo sio kana kwamba hajui kiswahili, anakijua vizuri kweli kweli kwa sababu si tumekua naye uswahilini na tunaishi naye huko jamani ila akifika kwenye kipaza sauti tu, basi yeye ni mtu wa yes and no kama hakijui vile Kiswahili.
Mtu huyo huyo ukimpeleka kwenye matangazo ya lugha ya kiingereza tupu hicho kitakachozunguzwa mdomoni mwake utaomba maji ya kunywa ila kwenye matangazo ya Kiswahili lazima atie maneno ya kiingereza, inakera jamani.
Ndugu zangu jueni kuwa vituo mnavyofanyia kazi vimesajiliwa kwa kurusha matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili pia watazamaji wenu au wasikilizaji wenu walio wengi hawajui hiyo lugha mnayoichombeza mara kwa mara kwenye matangazo yenu ya vipindi vya michezo au ya mpira ya moja kwa moja.
Ninaamini na nina hakika hakuna neno lolote la kiingereza ambalo halina maana kwa lugha ya Kiswahili hata hizo sheria na kanuni za soka zimetafsiriwa kwa lugha mbali mbali, ikiwemo hicho Kiswahili ambacho nyinyi mnakiona kama hakina thamani.
Nimekuwa nikitazama na kusikiliza matangazo ya moja kwa moja ya ligi kuu Tanzania bara iliyomalizika wiki moja iliyopita na moja ya kitu ambacho nilikuwa ninakerwa nacho tena kwa kiasi kikubwa ni hicho cha hao wachambuzi hasa hasa kuingiza maneno ya kiingereza kwa kiasi kikubwa kwenye kuuchambua mchezo husika.
Kwa kweli kwangu mimi ninaona kama ni umbumbumbu na kukosa uelewa tu wa mtu anayefanya hivyo na hilo limekuwa ni tatizo kubwa kwa watu wanaofanya hiyo kazi kwa sasa, yaani anatia neno la kiingereza hata sehemu ambayo unaona kabisa ina neno zuri tu kwa Kiswahili ila lazima aweke huo upuuzi wake.
Mwalimu wangu mmoja wa mambo ya utangazaji wa mpira wa miguu aliwahi kuniambia matangazo ya mpira yanavutia na kuleta ladha kubwa kwa msikilizaji au mtazamaji yanapotangazwa na mtu mzawa wa lugha husika hapa alikuwa na maana kama mtu anayetangaza mpira kwa Kiswahili itakuwa vyema akiwa mswahili mwenyewe yaani lugha yake ya asili ni kiswahili.
Aliendelea kusema kuwa kuna maneno mengine ya soka yanaeleweka na kuwavutia wale wenye lugha yao ya asili, kwa mfano unaweza kusema Mrisho Ngassa anapigwa daruga pale au mpira umeingia kwenye Kamba akiwa na maana mpira umeingia kwenye nyavu kwa maana hiyo kama wewe Kiswahili chako ni cha kujifunza unaweza usielewe haraka haraka au itachukua muda kuweza kuelewa maneno ya kisoka kwenye Kiswahili ila ukiwa mzawa utayajua na utafurahishwa nayo.
Hayo ni machache tu na ndio maana kila mtu au shabiki wa soka anavutiwa na matangazo ya mpira pale yanapotangazwa kwa lugha yake ya asili kwa sababu anaielewa vilivyo kushinda lugha ya kigeni, sasa ninawashangaa nyie mnaopenda kuingiza maneno ya kiingereza kwenye matangazo ya mpira na vipindi vya michezo huku lugha yenu ya asili ni Kiswahili.
Mbona Kiswahili kina maneno matamu sana na ya kuvutia tena yanapendwa sana na mashabiki wa soka ambao wengi wao wanawasikiliza na kuwatazama nyie kila kukicha ingawa mnajiona kama hamkijui vile kumbe ovyo kabisa wakati mmezaliwa na kukulia nchini Tanzania.
Nipo hapa China kwa muda mrefu kidogo sasa ila sijawahi kusikia mtangazaji au mchambuzi wa soka akiingiza maneno ya lugha ngeni au ya kiingereza kama watangazaji na wachambuzi wetu wa bongo na wanajivunia lugha yao kweli kweli sasa sijui sie watangazaji na wachambuzi wetu wamelogwa na nani.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved