SPIKA Anne Makinda ameitaka Serikali kuhakikisha bajeti ya mwaka
2015/16 inatekelezwa ipasavyo. Makinda alitoa kauli hiyo bungeni mjini
hapa jana wakati alipokuwa akiahirisha Bunge muda mfupi baada ya Waziri
wa Fedha Saada Mkuya Salum, kumaliza kusoma bajeti ya Serikali ya mwaka
2015/16.
Alisema: Hii ni bajeti ya mwisho kabla ya kuingia kwenye uchaguzi
mkuu, sisi tutafanya kazi yetu kadri inavyowezekana kuhakikisha bajeti
hii inatekelezeka, kipindi chetu karibu kinakwisha ila serikali
itakuwepo madarakani bado, hivyo tunaiomba utekelezaji wa bajeti hii,”
alisema.
Alisema bajeti hiyo itajadiliwa kwa muda wa siku 7 kwa wabunge kutoa
maoni yao, huku akiwataka wabunge ambao hawajajaza fomu kwa ajili ya
kupata nafasi ya kuchangia kufanya hivyo mara moja kwani bila hivyo
hawatapata fursa hiyo.
Aidha, Makinda aliwaonya wabunge kuacha kutukanana wakati wa mjadala
wa bajeti kwani si tabia njema na badala yake wajikite katika kuchangia
bajeti ya serikali ili kufikia malengo.
“Pia muache tabia ya utoro hata kama mna homa ya uchaguzi, ni vyema
kuhakikisha mnakuwapo muda wote wa mjadala. Katika hatua nyingine,
baadhi ya wabunge ametoa maoni tofauti ya bajeti huku wengine wakisifia
na wengine wakilalamika kuongeza tozo katika mafuta ya petroli, mafuta
ya taa na dizeli.
Mbunge wa Mtera, Livistone Lusinde (CCM) alisema yeye kama mbunge
anayewakilisha wananchi wa vijijini wenye kipato cha chini hawezi
kukubali serikali ikaongeza gharama kwenye mafuta, kwani hatua hiyo
itwaumiza zaidi wananchi wa vijijini.
“Pamoja na kuongeza tozo ya mafuta ni katika kuongeza mapato, lakini
itawaumiza watumiaji hususan wa vijijini na si wachakachuaji wa mafuta
hayo,” alisema na kusisitiza kuwa njia pekee ni kuweka adhabu kali kwa
wachakachuaji wa mafuta.
Naye Mbunge wa Kawe, Halima Mdee(Chadema) alisema kuongeza fedha
katika Mfuko wa Wakala wa Nishati vijijini ni jambo jema lakini kuna
haja ya kuhakikisha fedha hizo zinatolewa kwani katika bajeti ya mwaka
jana fedha zilizotengwa chini ya asilimia 50 ndizo zilizopelekwa REA.
Aidha, alionesha wasiwasi wake kwa wabunge kunyimwa meno katika
kupitia misamaha ya kodi kabla ya serikali kuikubali na kuipitisha, huku
akisema jambo hilo ni hatari kwani serikali inaongoza kwa kutoa
misamaha ya kodi.
Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM) alisema kitendo cha
kuongeza gharama kwenye mafuta ni kuwaumiza wanyonge na kusababisha
migomo isiyo ya lazima kwani hali hiyo itasababisha gharama za nauli
kupanda.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Zarina Madabida (CCM), alipongeza hatua
ya serikali kubadilisha mfumo na kuacha kuongeza bei kwenye pombe,
sigara, vinywaji baridi kama ilivyozoeleka miaka yote huku akisema
bajeti hiyo ni nzuri.
No comments:
Post a Comment