Spika atishia kukata posho kwa watoro

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi1vfnRn8Ssmg5TpmZaYdPi37dEkRP0v8lwZLuqDiSM5g1WHsRggwplby9PXZZfqRa-uB74XQEARu4iMxR5fRp51OlTc6vkTB7MOnq70X5h_b0A1BwE7SdI9AdKG_La75TMKV1s5pJa3qmA/s1600/DSC08448.JPG
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Pandu Ameir Kificho
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho ametishia kukata posho za wajumbe wa baraza hilo ambao watashindwa kuheshimu na kudhibiti nidhamu ya mahudhurio ya vikao hivyo vinavyoendelea.
Kificho alitoa kauli hiyo kutokana na mahudhurio hafifu ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika vikao vinavyoendelea vya kujadili makadirio mapato na matumizi ya bajeti za Wizara ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanatakiwa kuwa mfano mzuri wa kuonesha nidhamu ya utawala bora ikiwemo kuhudhuria katika vikao hivyo kwa wakati bila ya kukosa au kuwepo dharura maalumu ambayo Spika ataarifiwa.
Kificho alifafanua na kusema kwa masikitiko makubwa hivi sasa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanakuja na kukaa kwa muda mfupi na baadaye kuondoka moja kwa moja bila ya ruhusa ya Spika.
“Nimesikitishwa sana na mahudhurio hafifu ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika vikao vinavyoendelea...sisi wajumbe ndiyo tunaotakiwa kuwa mfano wa utekelezaji wa utawala bora kumbe sisi ndiyo wavunjifu wakubwa wa taratibu tulizojiwekea,” alisema.
Kificho alisema hivyo baada ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kushindwa kupitisha makadirio ya Wizara ya Elimu mara mbili baada ya kutokuwepo kwa akidi ya kutosha ya wajumbe kupitisha vifungu vya bajeti ya Wizara ya elimu na mafunzo ya amali.
Alisema kuanzia sasa atalazimika kutumia kanuni ya 158 ya utendaji wa kazi ambapo wajumbe watakaoshindwa kuhudhuria vikao hivyo bila ya taarifa ya spika au naibu spika watakatwa posho ya siku nzima.
Alisema kwamba vikao vya Baraza la Wawakilishi vimewekewa kalenda yake pamoja na bajeti yake kwa ujumla kwa hivyo wajumbe wanatakiwa kuheshimu ratiba hiyo ili vimalizike kwa wakati na kuepuka serikali kuingia katika gharama zisizokuwa na sababu.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved