
Hali hiyo ilifahamika jana jijini Mbeya wakati mmoja wa watangaza nia hao ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe kuutaarifu umati uliokuwepo kushudia tukio la kudhaminiwa kwake na wanachama wa mkoani Mbeya kuhusu msimamo wake wa kuungana na Prof. Mark Mwandosya.
Membe alisema wanaelewana vizuri na Prof Mwandosya ambaye pia ni Waziri wa Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, na kwamba yeyote kati yao atateuliwa na chama chao kukiwakilisha katika nafasi hiyo ya urais basi mwenzake atamuunga mkono.
Membe alimwelezea Prof Mwandosya kuwa mtu wake wa karibu na kwamba alimsaidia sana katika uchaguzi wa Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC ) ambapo yeye (Membe) aliwania nafasi hiyo kupitia kundi maarufu kwa jina la ‘kundi la kifo’.
“Napenda watu wajue kuwa natamka hili kwa moyo wangu wa dhati, jina langu lisiporudi ndani ya chama nitampigia kampeni Prof Mwandosya sina tatizo lolote hata wakisema mimi nimuachie Mwandosya nipo tayari kwani ndiyo viongozi wanaotakiwa kama yeye kwa sasa kuongoza nchi yetu,” alisisitiza Membe.
Akizungumzia nafasi yao, Membe alisema anatarajia kuwafanyia mambo makubwa wananchi wa Mbeya kama atapitishwa, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe kwa kuwa kitovu cha uchumi.
Alisema kuwa nchi za Ulaya zinapenda sana bidhaa ya maua na matunda ambayo wamekuwa wakiyategemea kutoka nchi ya Afrika Kusini, ambapo kwa Mkoa wa Mbeya bidhaa hiyo inapatikana hivyo ataunda tume maalumu ya kufanya utafiti katika mataifa mbali mbali yatakayoweza kuwekeza katika bidhaa hiyo kutoka Mbeya.
Alisema wakazi mkoani hapa wana bahati ya kuwa na uwanja wa ndege wa Kimataifa hivyo kabla hata ya kuapishwa kwake anatarajia kuunda kamati maalumu ya kushughulikia uchumi wa viwanda ambavyo vitahusika na usindikaji wa maua, matunda na mboga na kusafirishwa kwenda nje ya nchi kupitia fursa ya uwepo wa uwanja huo.
Membe ni mwanachama wa tano kufika mkoani Mbeya kwa ajili ya kutafuta wadhamini katika mbio zake hizo za kuwania nafasi ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Awali, Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Mwandi Kundya, alisema jumla ya wanachama 877 walijitokeza kumdhamini Membe na kwamba nani anafaa uwamuzi upo mikonini mwa wanachama. Membe apata wadhamini 5,000 Ruvuma.
No comments:
Post a Comment