Watu 16 wauawa katika mlipuko wa bomu Nigeria
Watu 16 wameripotiwa kuuawa katika mlipuko wa bomu uliotokea jana usiku
nchini Nigeria. Kwa mujibu wa duru za jeshi na hospitali nchini humo,
shambulio hilo lilitokea katika soko lililokuwa limefurika watu katika
jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria. Mbali na watu 16 kuuawa,
wengine kadhaa wamejeruhiwa baadhi wakiwa mahututi. Hadi sasa hakuna
kundi lolote lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo, ingawa kama kawaida
lawama zimeelekezwa kwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram
ambalo limekuwa likitekeleza vitendo kama hivyo. Hayo yanajiri katika
hali ambayo makamanda wa jeshi la Nigeria walikutana jana na makamanda
wenzao wa nchi nne jirani na taifa hilo kwa ajili ya kujadili njia za
kukabiliana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram. Maafisa hao
wa jeshi la Nigeria walikutana mjini Abuja, mji mkuu wa nchi hiyo na
makamanda kutoka Cameroon, Niger, Chad na Benin ambapo pamoja na mambo
mengine walikubaliana kuanzisha kikosi cha eneo kitakachokuwa chini ya
Umoja wa Afrika kwa lengo la kuliangamiza kabisa kundi hilo la kigaidi.
Mbali na hayo serikali ya Nigeria pia imehamishia kituo cha uongozi wa
kijeshi huko Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno, ambalo ni ngome
ya kundi hilo ili kukabiliana vilivyo na wapiganaji wa Boko Haram.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment