KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema anakiandaa kikosi
chake kwa ajili ya michuano yote na siyo michuano ya Kombe la Kagame,
huku leo akitarajiwa kuikabili SC Villa ya Uganda katika mechi ya
kirafiki.
Pluijm alisema anaijua michuano ya Kagame inayoanza Julai 11, mwaka
huu, lakini anaichukulia kama mazoezi yatakayowapa nguvu za kutetea
ubingwa wao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara pamoja na michuano ya Ligi ya
Mabingwa Afrika itakayoanza mapema mwakani.
“Maandalizi yetu siyo kwa ajili ya Kagame, bali ni michuano yote
ambayo inatukabili mbele yetu lengo letu ni kufanya vizuri katika kila
michuano ndio maana unaona tumeanza maandalizi mapema na hata zoezi la
usajili tumefanya kwa haraka ili tuweze kutimiza kile ambacho
tumekidhamiria,” alisema Pluijm.
Alisema anajua timu nyingi zitaka zoshiriki Kagame zitakuwa
zimejiandaa kutokana na ubora waliokuwa nao kwa siku za karibuni, lakini
hilo halimuumizi kichwa kwani ana matumaini ya kutwaa ubingwa huo na
kujiwekea historia nyingine akiwa na Yanga.
Alisema anasema hivyo kwa sababu Yanga ndiyo timu pekee yenye kikosi
bora Afrika Mashariki na Kati na hilo atalidhihirisha kwenye michuano ya
mwaka huu itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Pluijm ameweka wazi kuwa hamtamsajili kiungo
Lansana Kamara wa Sierra Leone kutokana na kutoridhishwa na kiwango
chake katika mazoezi ya wiki mbili aliyofanya na timu hiyo.
Alisema uwezo wa kiungo huyo hauna tofauti na baadhi ya wachezaji
wazawa hivyo ameona nibora akaachana na mchezaji huyo kwa kuwa hana
vigezo vya aina ya mchezaji aliyekuwa akimuhitaji kwa ajili ya kuisaidia
timu yake katika michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa watakayoshiriki
mapema mwakani.
Katika hatua nyingine, Yanga leo wanashuka dimbani kwenye Uwanja wa
Taifa Dar es Salaam kuchuana na Sports Club Villa ya Uganda ikiwa ni
mchezo wa kwa wa kimataifa wa kirafiki.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda atakuwa mgeni rasmi katika pambano la
miamba hiyo miwili ya Afrika Mashariki na Kati ambalo litakuwa ni
maalumu kwa ajili ya kuwachangia watu wenye mahitaji maalumu.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha aliliambia gazeti hili kuwa
katika mchezo huo watawashtukiza mashabiki kwa kuwaletea wachezaji ambao
hawajaona.
Miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa ni Mzimbabwe Donald Ngoma ambaye
Yanga ilimtaja siku za karibuni kuwa ni mchezaji wanayemhitaji.
No comments:
Post a Comment